Wageni kutoka Tanzania kuwekwa karantini Mombasa

Wageni kutoka Tanzania kuwekwa karantini Mombasa

WINNIE ATIENO na IAN BYRON

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imebuni mikakati mipya ya kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona huku visa vikiongezeka nchini.

Katika mikakati hiyo, wageni kutoka nchi jirani ya Tanzania wasiokuwa na vyeti vinavyoonyesha hawana virusi hivyo watawekwa karantini ya lazima.

Kamati maalum ya dharura inayoshughulikia maswala ya corona Mombasa, ilitaja magari ya umma, kivukio cha feri, tuktuk na bodaboda kuwa mojawapo ya sehemu hatari kwa maambukizi ya corona.

“Kama kamati tumeamua kuanza kukaza kamba kwa sababu tumehsuhudia ulegevu miongoni mwa wakazi. Lazima kila mtu na wafanyibiashara wote wafuate kanuni,” alisisitiza gavana Hassan Joho ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo.

Kamati hiyo pia ilipendekeza safari za usiku kwa kutumia reli ya SGR na ndege kukaguliwa kwani inahitilafiana na kafyu.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Gilbert Kitiyo, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo alisema abiria wa SGR wanakiuka sheria za kudhibiti maambukizi kwa kusongamana.

Kwingineko, Gavana wa Migori, Bw Okoth Obado ameagiza mochari zote za kaunti hiyo zifungwe.

Bw Obado, ambaye alikuwa akihutubu nyumbani kwake, alisema miili itakayoruhusiwa kuhifadhiwa kwa muda mfupi katika mochari ni ya watu ambao wataaga dunia wakiwa hospitalini.

Alisema hatua hiyo imelenga kuepusha matanga ambayo huvutia idadi kubwa ya watu wanaoandaa mazishi kwa muda mrefu, na kuweka watu katika hatari ya kuambukizana virusi vya corona.

“Wale wanaofariki wakitibiwa wanafaa kuzikwa baada ya siku mbili. Hospitali na mochari za kibinafsi ambazo zitakiuka agizo hili zitapokonywa leseni,” akasema.

Pia alitaka kila anayeandaa mazishi, ibada na sherehe kama vile harusi wafuate kanuni zilizotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Kavindu aapishwa rasmi kuwa Seneta wa Machakos

57 kuosha jiji kwa kukiuka kanuni za Covid