Wageni wakoroga starehe za vigogo wa zamani ODM

Wageni wakoroga starehe za vigogo wa zamani ODM

Na WAANDISHI WETU

MAKABILIANO yameanza kuibuka kati ya wanasiasa wanaodai wamekuwa waaminifu kwa Chama cha ODM kwa muda mrefu, na wandani wa zamani Kiongozi wa Chama Raila Odinga ambao walirudi katika chama hicho hivi majuzi.

Huku chama hicho kikiashiria kuwa baadhi ya maeneo hayatafanyiwa kura ya mchujo ila wajumbe ndio wataamua anayestahili kupewa tikiti, wanachama ambao wamekaa katika chama hicho kwa muda mrefu sasa wanalazimika kutetea uaminifi wao kwa chama dhidi ya wenzao ambao wanaonekana kama wageni chamani.

Kulingana na maafisa wa ODM, chama hicho hutegemea vigezo tofauti iwapo kuna hitaji la kumpa mwaniaji tikiti moja kwa moja bila kupitia kwa kura ya mchujo.Vigezo hivyo ni kama vile uaminifu wa mwanasiasa kwa misimamo ya chama, na uwezo wa mwanasiasa kuzoa kura nyingi dhidi ya wapinzani wake wa vyama pinzani.

Kivumbi kinashuhudiwa sana baina ya wanasiasa wanaomezea mate viti vya ugavana kupitia kwa ODM.Katika Kaunti ya Mombasa, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir anatarajiwa kushindania tikiti hiyo dhidi ya Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi na mfanyabiashara Suleiman Shahbal.

Katika kaunti jirani ya Kilifi, Naibu Gavana Gideon Saburi anatarajiwa kushindania tikiti ya ODM dhidi ya Waziri wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro kuwania urithi wa kiti cha Gavana Amason Kingi.Huko Taita Taveta, Gavana Granton Samboja amekuwa akionyesha nia ya kutaka kuingia ODM kwa muda mrefu sasa, huku tikiti ya chama hicho ikimvutia pia Mbunge wa Mwatate, Bw Andrew Mwadime ambaye ni mwanachama wa ODM.

Mjini Mombasa, Bw Nassir na Dkt Kingi wamekuwa chamani kwa muda mrefu, huku Bw Shahbal akijiunga na chama hicho mapema mwaka huu baada ya kuhama Jubilee.Mfanyabiashara huyo alikuwa ametumia Jubilee kuwania ugavana 2017, na alitumia Wiper kuwania kiti hicho hicho mwaka wa 2013.

Alishindwa na Gavana Hassan Joho wa ODM katika chaguzi hizo.Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Nassir alisema hana wasiwasi kuhusu mfumo wowote ambao ODM itatumia kuamua atakayepeperusha bendera katika uchaguzi wa ugavana kwa kuwa anaamini yeye ndiye anastahili.

“Bw Odinga alipoongea Likoni aliambia watu wasihame ODM wakati watakaposhindwa katika kura ya mchujo jinsi wamezoea kufanya. Mimi sikuwa katika mkutano huo, nilikuwa naomboleza. Bw Odinga alikuwa akiongea na wale ambao walikuwa katika mkutano huo.

Tunajua ni kina nani wana mazoea ya kuhamahama vyama,” akasema Bw Nassir. Hata hivyo, Bw Shahbal alisema hatarajii kutakuwa na mapendeleo yoyote chamani kupeana tikiti. “Bila shaka tutashinda tikiti hii.

Acha hao wapinzani wangu wawili (Bw Nassir na Dkt Kingi) watafute nafasi nyingine. Tunatarajia uteuzi utafanywa kwa njia ya haki kwani kiongozi wa chama alituhakikishia hilo na tuna hakika tutashinda,” akasema Bw Shahbal.

Mfanyabiashara huyo alipuuzilia mbali wanaotilia shaka uaminifu wake kwa Bw Odinga katika hotuba za awali. Alisema ukaribu wake na waziri huyo mkuu wa zamani umevuka hata mipaka ya kisiasa.

Bw Odinga alimkaribisha rasmi Bw Mung’aro chamani wakati wa mkutano wa hadhara Kilifi alipokuwa ziara ya Pwani hivi majuzi.Bw Mung’aro alikuwa amewania ugavana kupitia Chama cha Jubilee mwaka wa 2017, lakini awali alikuwa mwanachama wa ODM.

Alikosoa wanaomtaja kuwa mgeni katika ODM na kusema alikuwa mmoja wa wanachama waliotangulia kuingia chama hicho kilipoanzishwa na wakakivumisha Pwani akiwa na Waziri wa Utalii Najib Balala, ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Mvita.

Naibu Gavana Saburi, alisema hababaishwi na hatua ya Bw Mung’aro kurudi ODM akisema atakuja na wafuasi wake na hilo litaimarisha chama.Aliongeza kuwa, ana uwezo wa kutosha kupambana naye katika uteuzi ili ashinde tikiti ya kuwania ugavana.

“Tutaenda mchujo na mwenzangu Mung’aro na nina hakika mimi ndiye nitakuwa Gavana wa Kilifi baada ya uchaguzi 2022,” akasema.Katika Kaunti ya Taita Taveta, Bw Samboja amekuwa akihudhuria mikutano ya ODM na kupuuza ile ya Wiper huku pia akifanya mikutano ya faraghani na Bw Odinga, ila hajatangaza rasmi nia ya kuhepa chama cha Kalonzo Musyoka.

Kwa upande wake, Bw Mwadime alichaguliwa kupitia kwa ODM mwaka wa 2013 na 2017. Ameibuka kuwa mmoja wa wafuasi waaminifu wa chama hicho na Bw Odinga, katika ukanda wa Pwani.“Nina uwezo wa kushinda tikiti ya chama hicho na hatimaye ugavana 2022.

Niko tayari kwa kinyang’anyiro uchaguzini,” Bw Mwadime alisema katika mahojiano ya hivi majuzi.Ripoti za Winnie Atieno, Siago Cece na Lucy Mkan

You can share this post!

Polisi wakosa kunasa wezi wa benki Kisumu

Wahudumu ufuoni waanza kupewa chanjo

T L