Habari Mseto

Wagiriama warejeshewa sanamu zilizokuwa zimefichwa Uingereza

July 30th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

WAZEE wa Kaya katika jamii ya Wagiriama Jumatatu walishukuru serikali za Kenya na Marekeni kwa kuwarudishia baadhi ya sanamu za viongozi wao zilizoibwa miaka ya 60 na 70 na kupelekwa Uingereza.

Walisema hatua hiyo itaipa jamii ya Wagiriama utulivu.

Waziri wa Utamaduni, Michezo na Turathi za kitaifa Bi Amina Mohammed aliongoza hafla ya kuwakabidhi wazee hao sanamu hizo.

Vigango hivyo ambavyo vilikuwa 41 vilikuwa vimehifadhiwa katika makavazi ya Denver baada ya kuchukuliwa nchini na kuuzwa kama bidhaa za sanaa.

Mwenyekiti wa chama cha utamaduni, Bw Joseph Mwaradandu alisema awali watu walikuwa wakiiba vigango na kuviuza kwa watu wa mataifa mbalimbali.

“Hizi si mbao bali ni mizimu ya wazee wetu. Hawa hawafai kuwa mahali pengine popote isipokuwa nyumbani. Wanapotenganishwa na jamaa zao masaibu makubwa hukumba jamii hizo. Kwa mfano, kuna watu watashikwa na wazimu ama wanyama kufariki, njaa na ukame hadi pale watakaporejeshwa,” akasema.

Bi Mohammed alisema serikali itaendelea na juhudi za kuhakikisha turathi zote zilizochukuliwa na mataifa mengine zinarudishwa ili kuendeleza utamaduni wa jamii za Kenya.