Wagombea wa UDA, Jubilee eneobunge la Kiambaa wawarai wafuasi wao wajitokeze

Wagombea wa UDA, Jubilee eneobunge la Kiambaa wawarai wafuasi wao wajitokeze

Na SAMMY WAWERU

UCHAGUZI mdogo wa kiti cha ubunge Kiambaa unaendelea, mgombea wa UDA John Njuguna Wanjiku na Jubilee, Kariri Njama wakiwa tayari wamepiga kura zao.

Wawaniaji hao walipiga kura dakika chache baada ya saa tano asubuhi, Jumanne, ambapo walikuwa wameandamana na baadhi ya wanasiasa.

“Ninahimiza wale ambao hawajapiga kura wahakikishe wamejitokeza,” akasema Bw Njuguna, na ambaye alikuwa ameandamana na mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua.

Kwa upande wake Bw Gachagua, alieleza kuridhishwa kwake na hali ya usalama ilivyoimarishwa.

Bw Kariri Njama alikuwa ameandamana na mbunge wa Kieni, Kanini Kega na mwakilishi wa wanawake Murang’a, Bi Sabina Chege.

“Uchaguzi umeanza vizuri na ninaomba wapigakura wajitokeze kwa wingi,” Bw Njama akasema.

Kinyang’anyiro hicho kimevutia wagombea wanane.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanahisi uchaguzi mdogo wa Kiambaa ni mizani ya umaarufu kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto eneo pana la Mlima Kenya.

Chama cha UDA kinahusishwa na Dkt Ruto.

Kiti cha ubunge Kiambaa kilisalia wazi Machi 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge Bw Paul Konange.

You can share this post!

Shikanda asema ladha ya ligi iliisha Juni 30

Jinsi ya kuandaa meatballs