Mistari ya mwisho

Mistari ya mwisho

NA CECIL ODONGO

WAWANIAJI wanne wa urais nchini jana Jumamosi waliandaa mikutano ya mwisho kusaka uungwaji mkono huku wakitoa ahadi tele na kuwaomba Wakenya wawapigie kura katika Uchaguzi Mkuu wa Jumanne.

Naibu Rais Dkt William Ruto wa UDA na Mwaniaji wa Urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, waliandaa mikutano mikubwa ya kisiasa katika viwanja vya michezo vya Nyayo na MISC Kasarani mtawalia.

Wagombeaji wa Urais Profesa George Wajackoyah wa Roots Party na David Mwaure wa Agano Party pia walikuwa jijini Nairobi.

Profesa Wajackoyah aliandaa msururu wa mikutano mitaani Westlands, Deap Sea, Masari Hill na Highridge.

Bw Mwaure naye aliandaa mkutano na viongozi wa kidini katika kanisa Katoliki la St Teresa, mtaani Eastleigh ambapo alijinadi kama kiongozi mwenye suluhu kwa changamoto zinazoikabili nchi.

Rais Uhuru Kenyatta naye hakuachwa nyuma, kwa kuwa alikuwa na mikutano kadha ya kampeni katika Kaunti ya Nyeri alikowarai raia wajitokeze na kumpigia Bw Odinga pamoja na mgombeaji mwenza wake, Martha Karua mnamo Jumanne.

Akizungumza katika makao yake mtaani Karen, Nairobi kabla ya kuelekea Narok na Nyayo, Dkt Ruto alitoa wito kwa Wakenya wamchague, akisema serikali yake itawakomboa raia kutoka maisha magumu pamoja na kuwavutia wawekezaji nchini.

“Maisha hayajawahi kuwa magumu kiasi hiki nchini, inasikitisha Wakenya hawawezi kuweka chakula mezani. Nikichukua usukani baada ya uchaguzi wa Jumanne, kazi ya kwanza ambayo nitafanya ni kuweka mikakati ya kiuchumi kuwaokomboa Wakenya,” akasema Dkt Ruto.

Hasa, alinadi mpango wake wa kiuchumi maarufu kama ‘Bottom Up’, akiahidi kutenga Sh50 bilioni kwa vijana wasiokuwa na ajira.

Dkt Ruto pia alisema ziara zake kote nchini, zimemwezesha kubaini matatizo kwenye kaunti mbalimbali ambayo atayashughulikia akiwa Rais.

Kuhusu uchaguzi wa Jumanne, Dkt Ruto aliwataka wafuasi wake wasitishike na baadhi ya maafisa wa serikali aliodai wanapanga njama ya kuiba kura, akisema raia ndio wataamua mshindi wa uchaguzi huo.

“Tunawaomba Wakenya wajitokeze kwa wingi ili kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia. Tunawaomba mkatae kutishwa, kuhongwa na kuamini matamshi yaliyojaa uongo. Tafadhali msikubali kutishwa,” akasema Dkt Ruto.

Akiwa ameandamana na vinara wa Kenya Kwanza, Dkt Ruto, kwa mara nyingine alidai serikali inapanga kuwatumia machifu kumuibia Bw Odinga kura na kuitaka IEBC ihakikishe kuna uwazi katika shughuli hiyo.

Bw Odinga naye akiwahutubia wafuasi wake, alijirejelea kama mkombozi wa Wakenya, akiahidi kupambana na ufisadi, kubuni nafasi za ajira, kuzipa familia zisizojiweza Sh6,000 na pia kuhakikisha uchumi wa Kenya unanawiri.

“Natoa ahadi kuwa nitawekeza rasilimali kwa wananchi wa Kenya ambao ni tegemeo letu. Tumekuwa taifa la wananchi wengi wenye shida ya kukimu maisha yao na wachache wenye kufaidi maisha ya raha. Natoa ahadi ya kupambana na umasikini kwa kumfanyia haki kila mtu bila kulibagua kundi lolote,” akasema Bw Odinga.

Awali, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, alizindua manifesto ambayo ilitaja mipango ya maendeleo itakayotekelezwa na muungano wao katika maeneo 11 nchini iwapo watafanikiwa kutwaa mamlaka.

“Tulizindua manifesto ya kitaifa na kwa kuwa nchi ina matatizo mbalimbali, tulibaini changamoto kwenye kila kaunti kisha kupendekeza utatuzi. Manifesto hii inajikita katika kuimarisha uchumi wa maeneo hayo,” akasema Bw Oparanya.

Aidha, Bw Odinga aliwataka wafuasi wake wasichoke na kukataa tamaa kuwa atapokonywa ushindi na badala yake wote wajitokeze na kumpigia kura.

Alikashifu kambi ya Dkt Ruto na kuitaja kuwa na wanasiasa wanaowahadaa, ambao hawana uwezo wa kuyabadili maisha yao kutokana na kuhusishwa na sakata mbalimbali za ufujaji mali ya umma awali.

Rais Uhuru Kenyatta naye alimpigia debe Bw Odinga akiwataka wakazi wa Mlima Kenya wamchague ili wasiachwe nje ya serikali ya Azimio la Umoja.

Pia aliwataka wawachague tu wale ambao wanawania vyeo Jubilee.

“Ni Raila na Martha. Hivyo ndivyo mambo yalivyo. Nyinyi watu wa Othaya, msikubali kuachwa nje ya serikali. Wale wanaozunguka wakinitukana, wanajua kuwa Wakenya washaamua. Na mimi sitawajibu,” akasema.

Baada ya muda wa kampeni kutamatika jana Jumamosi, kanuni za IEBC zinawazuia wanasiasa kuendelea na mikutano ya umma huku kilichosalia sasa ni raia waelekee debeni mnamo Jumanne na kutekeleza wajibu wao wa kidemokrasia.

Habari zaidi na Mwangi Ndirangu

  • Tags

You can share this post!

Tottenham wapepeta Southampton 4-1 katika EPL

Borussia Dortmund wakomoa Leverkusen katika Bundesliga

T L