Wagonjwa 18 wa corona wafa moto ulipozuka kwenye wodi

Wagonjwa 18 wa corona wafa moto ulipozuka kwenye wodi

Na MASHIRIKA

WAGONJWA 18 walifariki baada ya moto kutokea katika wodi ya wagonjwa wa Covid-19 katika hospitali moja magharibi mwa India huku nchi hiyo ikiandikisha rekodi nyingine ya maambukizi mpya duniani, ya visa 401,993 jana pekee.

Wagonjwa wengine 3,523 walifariki ndani ya saa 24 zilizopita katika nchi hiyo ambayo kufikia sasa imeandikisha jumla ya visa 19.1 milioni ya maambukizi ya corona.

Kufikia jana, India ilikuwa imeandikisha jumla ya vifo 211, 853 kulingana na takwimu za wizara ya afya, ambazo wataalamu wanashuku ni juu zaidi.Moto wa jana ulitokea katika wodi hiyo iliyoko orofa ya kwanza lakini ukazimwa baada ya saa moja, kulingana na taarifa kutoka makao makuu ya polisi.

Chanzo cha moto huo kinachunguzwa.Polisi walisema moto huo ulitokea usiku wa kuamkia jana katika wadi ya wagonjwa mahututi katika Patel Welfare Hospital, ilitengwa mahsusi kwa waathiriwa wa Covid-19.

Hospitali hiyo iko mji wa Bharuch, kilomita 185 kaskazini mwa jiji kuu la jimbo, Ahmedabad.  “Wagonjwa 16 na wafanyakazi wawili wamefariki katika mkasa huo wa moto. 12 kati yao waliteketea na kuzongwa na moto,” akasema RV Chudasama, ambaye ni mkuu wa polisi jijini Bharuch.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa moto huo ulisababisha na hitilafu kwenye nyaya za umeme,” akaongeza.Lakini Dushyant Patel, afisa wa serikali, alidai kuwa moto huo ulisababishwa na kufuja kwa mtungi wa oksijeni katika wadi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi.

Vyombo kadha vya habari vilionyesha picha za wodi ya hospitali hiyo ikiwa imeharibiwa kabisa.“Moto huo ulivuruga shughuli katika hospitali hiyo. Wafanyakazi waliwaondoa watu wa familia yangu kutoka wadi hiyo na tukawahamisha hadi hospitali nyingine kwa kwenye gari letu,” akasema Parth Gandhi.

Jamaa zake wawili ambao ni wanaugua corona walinusurika katika mkasa huo.Waziri Mkuu Narendra Modi alisema kupitia ujumbe wa twitter kwamba “Nimetamaushwa zaidi na maafa yaliyotokea katika mkasa wa moto katika hospitali moja mjini Bharuch.”

Wagonjwa 31 wengine katika hospitali hiyo waliokolewa na wafanyakazi pamoja na wazima moto na hali yao ni shwari, alisema afisa wa polisi BM Parmar.

Mnamo Aprili 23, moto uliotokea katika kitengo cha kuwahudumia wagonjwa mahututi ulisababisha vifo vya wagonjwa 13 wa Covid-19 katika eneo la Virar viungani mwa jiji la Mumbai.

You can share this post!

Serikali ya TZ sasa yaweka mitambo ya oksijeni hospitalini

DCI yaonya wasichana dhidi ya walaghai mtandaoni