Habari Mseto

Wagonjwa wa corona wanaojitokeza wasifiwa

July 21st, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Wanaojitokeza na kufichua kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 wanaimarisha kampeni ya kupambana na kero la unyanyapaa katika jamii.

Wizara ya Afya imesema hatua ya baadhi ya viongozi na watangazaji kujitokeza hadharani na kueleza wameambukizwa virusi vya corona inatia motisha kwa Wakenya wanaohofia kuwa ugonjwa huu ni tiketi ya maafa.

“Ni jambo la kutia moyo kuona watu walioshikilia nyadhifa kuu serikalini na wasanii wenye ushawishi mkubwa nchini kama vile watangazaji wakijitokeza na kufichua wameambukizwa Covid-19. Hii ni njia mojawapo kupambana na kero la unyanyapaa kwa walioambukizwa katika jamii,” akasema Waziri Msaidizi katika wizara Dkt Rashid Aman.

Mtangazaji maarufu Jeff Koinange na ripota Stephen Letoo, ni kati ya waliojitokeza hivi karibuni na kufichua wameambukizwa corona.

Kulingana na Dkt Aman ujasiri wa wanahabari hao unaonyesha Covid-19 ni ugonjwa kama mengine, na unaoponwa. “Ugonjwa huu si tiketi ya kifo, tumeona watu wengi walioambukizwa wakipona. Tuwape motisha waliopatwa na virusi vya corona, watapona,” Waziri akaelezea.

Alihimiza taasisi, kampuni na vyombo vya habari ambavyo wafanyakazi wake wanapatikana na corona kualika wizara ya afya kufanya vipimo kwa kila mmoja.

Hata hivyo, alisema ni wajibu wa idara ya afya kufuatilia waliotangamana na waathiriwa. “Vyombo vya habari ambavyo wafanyakazi wake wameathirika vifanye vipimo kwa kila mfanyakazi ili kudhibiti kusambaa zaidi miongoni mwao,” akashauri Dkt Aman.