Habari

Wagonjwa wanafariki tukitazama, serikali iwajibike – Madaktari

April 24th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

MADAKTARI katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru Level Five wamekiri kuwa wagonjwa wamekuwa wakifariki humo kutokana na subira ya muda mrefu bila kuhudumiwa.

Madaktari hao walisema kuwa wagonjwa wanaofika kwenye kifaa hicho cha afya wamekuwa wakisubiri kati ya siku mbili na tatu bila kuhudumiwa, jambo ambalo limesababisha vifo vya watu wengi.

Taarifa hizo za kushtua zimerejesha kumbukumbu za malalamishi ambayo yamekuwepo kuwa wagonjwa katika hospitali hiyo wamekuwa wakipokea huduma mbovu.

Madaktari hao walilaumu uhaba  wa wafanyakazi kwa matatizo yao, wakidai kuwa japo ni hospitali ya rufaa, imekuwa ikifanya kazi kama zahanati.

Baadhi ya sehemu walizosema zimeathirika ni wanakozalia kina mama, sehemu za kufanyia upasuaji, kunakopigiwa picha za X-rei na sehemu za wagonjwa mahututi.

Walisema hayo walipotoa ilani ya mgomo utakaoanza wiki ijayo, wakilalamikia uhaba wa madaktari katika kaunti hiyo, kukosa kupandishwa vyeo kwa muda mrefu na kunyimwa bima ya afya.

 

‘Hatuwezi kuwasaidia’

“Wagonjwa wanaaga dunia kila uchao tukitazama kwani hatuwezi kuwasaidia. Baadhi ya wagonjwa wanakaa kati ya saa 48 na 72 bila kumwona daktari,” akasema Dkt Davji Atellah.

Daktari huyo alisema kuwa japo hospitali hiyo inayowahudumia wakazi wa kaunti sabaa kwa kuwa ni ya rufaa inafaa kuwa na zaidi ya madaktari 200, kwa sasa ina 20 pekee.

Madaktari hao walizidi kusema kuwa upungufu wa madaktari umepelekea baadhi ya idara kuwa na mtaalamu mmoja pekee, ilhali idadi ya wagonjwa wanaotafuta huduma ni kubwa kupita kiasi.

Walisema japo serikali ya kaunti ilinunua vifaa vya afya na kupeleka katika kifaa hicho, vimesalia kuwa maridadi tu kwa kuwa hakuna wafanyakazi wa kuvitumia.

Hii, walisema, ni licha ya hospitali nyingine kaunti hiyo kukumbwa na matatizo sawa, wakisema ile ya Subukia Level Four ina wodi zisizotumika kutokana na ukosefu wa madaktari na wahudumu wengine.

 

Miaka 4 bila likizo

Baadhi ya madaktari walieleza Taifa Leo kuwa wamekaa zaidi ya miaka minne bila kwenda likizo wala kupata siku za kupumzika, wakisema hali hiyo iliadhiri utendakazi wao na maisha yao ya kifamilia.

“Tunajua si haki kwetu kugoma kila wakati kwani hatukwenda shuleni ili tuwe tukigoma lakini serikali inatusukumia kufanyia kazi katika mazingira magumu sana na hali hii inatuweza sasa,” akasema Dkt Carolyne Masete.

Walizidi kulalamika kuwa kaunti hiyo haijafanya zoezi la kupandisha madaktari mamlaka tangu 2015, suala walilosema limeadhiri utendakazi wao.

Hii, walisema, ni licha ya wengi wao kunyimwa bima ya afya, ambayo walisema ni haki yao.

“Kwa sababu hizi, kuanzia Mei 3, madaktari kaunti hii watagoma ili kupigania tupewe haki zetu za kufanyia kazi katika mazingira mema,” akasema Dkt Atellah.

Hata hivyo, mkuu wa hospitali ya Nakuru Level Five Joseph Mburu alipinga madai ya wagonjwa kufia katika kifaa hicho kwa kukosa kupewa huduma, akiyataja kuwa yenye makosa na ya uongo.

“Tuna vifaa vyote vya kuwahudumia wagonjwa kuanzia wanapoingia hospitalini hadi wanapofikishwa kwenye wodi, na wanapofika humo hawamalizi dakika 15 bila kuonwa na mhudumu wa afya,” akasema Dkt Mburu.