Habari Mseto

Wahadhiri: Tutagoma hadi tupewe haki yetu

April 10th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Miungano ya Vyama vya Wahadhiri na Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu nchini Jumatatu walisisitiza kwamba mgomo wao bado unaendelea hadi pale serikali kuu itawatimizia mapendekezo kwenye makubaliano ya 2017-2022.

Katibu mkuu wa Muungano wa Wahadhiri (UASU) Constantine Wasonga (pichani kati), mwenzake wa Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) Charles Mukhwana na Mwenyekiti wa UASU Muga K’olale wamesisitiza serikali haijajitolea kikamilifu kuhakikisha mgomo huo unasitishwa.

Wakizungumza na wanahabari wakiwa wameandamana na viongozi wengine, walisema kwamba suala la kusitisha ama kuendelea kwa mgomo huo linashughulikiwa na mahakama baada ya kuwasilisha rufaa kupinga uamuzi uliowataka kurejea kazini.

“Sisi hatutazungumzia suala tata linaloshughulikiwa mahakamani jinsi alivyoshauri jaji mkuu David Maraga wiki jana lakini kile tunapigania ni kujadiliwa na kutekelezwa kwa mwafaka wa 2017-2022”, akasema katibu wa UASU Constatine Wasonga.

Aidha, alitaka serikali kukoma kutoa vijisababu ambavyo havina mashiko na badala yake itafute njia za dharura kuhakikisha mgomo huo unaisha ili zaidi ya wanachuo 600,000 warejee darasani.

Hata hivyo, viongozi hao walionekana kulegeza msimamo kuhusu kutekelezwa kwa muafaka huo huku wakitoa pendekezo nafuu kwa serikali.

“Iwapo serikali inaona muafaka wetu ni mzigo mkubwa kwa uchumi basi tunawapendekezea watulipe awamu ya mwaka mmoja na malimbikizi ya marupurupu yetu kisha pesa zinazosalia wazitenge katika bajeti ya miaka inayofuatia hadi mwaka wa 2021,” akasema katibu wa KUSU Charles Mukwana.

Alidai kwamba serikali ina njama fiche ya kutaka kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu nchini na kukishtumu Chuo kikuu cha Nairobi kwa kwenda mahakamani ili kushurutisha wafanyakazi na wahadhiri wake kurejea kazini.

“Chuo Kikuu cha Nairobi kinawalazimisha wanachama wetu kurudi kazini lakini tumekata rufaa kuhusu uamuzi uliotolewa na mahakama ya kuwataka wafanyakazi wa chuo hicho warejee kazini,” akasisitiza.

Viongozi hao walidai kwamba hazina kuu ya serikali imewatengea fedha ila serikali kuu ndiyo kikwazo kwa kutotoa idhini ya kutolewa kwa pesa hizo.
Pia, walikanusha habari kwamba walikutana na waziri wa Leba Ukur Yatani wiki jana kwa majadiliano kuhusu kusitishwa mgomo huo.

Viongozi hao walitarajiwa kukutana na Waziri wa Elimu Amina Mohamed jana na kisha kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu Elimu siku ya Alhamisi kujaribu kutafuta suluhu ya kumalizika kwa mgomo huo ambao umedumu kwa wiki sita hadi sasa na kulemeza shughuli za masomo kwenye vyuo 31 vya umma.