Habari Mseto

Wahadhiri waapa kutumia njia zote kuendeleza mgomo wao

April 19th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

WAHADHIRI wa vyuo vikuu vya umma Jumatano waliapa kutumia njia mbadala kuendeleza mgomo wao baada ya maandamano waliyopanga kufanya kusambaratishwa na polisi jijini Nairobi.

Wahadhiri hao walikuwa wakielekea katika makao makuu ya Wizara ya Elimu na Hazina ya Kitaifa jijini Nairobi, ila maandamano yao yakazimwa na polisi walipofika katika Jumba la Anniversary.

Aidha, walikuwa wamekusanyika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, walikolalamikia kutojitolea kwa serikali katika kusuluhisha mgomo wao. Licha ya hayo, polisi waliingilia kati na kuwazuia, wakishikilia kwamba hawakuwa wamepokea notisi ya kuwakubalia kuandamana.

Polisi waliokuwa wamejihami vikali walidai kupokea “maagizo kutoka juu” walitishia kuwarushia vitoa machozi, iwapo hawangetii maagizo yao.

“Hatujapata kibali rasmi kuruhusu maandamano yoyote. Hivyo, lazima wanaondamana waondoke barabarani mara moja,” akasema Mkuu wa Polisi katika Kituo cha Central, Robinson Thuku, aliyeongoza kikosi hicho.

Ilibidi wahadhiri kurejea katika Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako waliapa kutumia kila njia kuhakikisha kwamba hakuna shughuli zozote za masomo zinaendelea katika vyuo hivyo, hadi pale matakwa yao yao kushughulikiwa.

Wahadhiri hao wanashinikiza kutekelezwa kwa Mwafaka wa Malipo wa 2017-2021, ili kuongezwa mishahara na marupurupu wanayopata.

Kwenye hotuba zao, viongozi wa Chama cha Wahadhiri (UASU) na Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) waliwalaumu Waziri wa Elimu Amina Mohamed na Katibu Japeh Ntiba kuwa kikwazo kikuu cha kupatikana kwa suluhisho kuu.

Mwenyekiti wa UASU Prof Muga K’Olale alisema kuwa wawili hao hawana ufahamu wa kindani kuhusu malalamishi halisi ya wahadhiri na wafanyakazi wengine, kwani wameluwa wakikubali kupotoshwa na Manaibu Chansela (VCs).

Prof K’Olale alisema kwamba juhudi za kuwafikia wawili hao zimegonga mwamba, hivyo wakibaki bila lingine ila kuendeleza mgomo huo.

“Nimekuwa katika harakati za kuwatetea wafanyakazi wa vyuo vikuu kwa muda mrefu, ila kinyume na migomo mingine, kikwzo kikuu kwa sasa ni waziri husika (Amina) kukubali kupotoshwa na wakuu wa vyuo kwamba hakuna ukweli wowote katika malalamishi yetu,” akasema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UASU Dkt Constantine Wasonga alisema kuwa wako tayari kumaliza mgomo huo, ikiwa serikali iko tayari kutoa mapendekezo yake kuhusiana na mkataba huo.

 

 

 

Mgomo huo ambao unaingia siku ya 49 leo umeathiri masomo katika vyuo vyote 31 vya umma nchini na wanafunzi zaidi ya 600,000.