Wahadhiri wapongezwa huku wakiahidi kuendelea kuweka MKU kwenye ramani

Wahadhiri wapongezwa huku wakiahidi kuendelea kuweka MKU kwenye ramani

NA LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kiliandaa hafla ya siku tatu jijini Nakuru ambapo wadau muhimu walitathmini jinsi ya kukisuka upya.

Hafla hiyo ya siku tatu ilihudhuriwa na mwanzilishi wa chuo hicho Profesa Simon Gicharu, Naibu Chansela Prof Deogratius Jaganyi na mwenyekiti wa kamati ya chuo Prof David Serem.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo walitoka  katika vitengo vya chuo hicho vya hapa nchini na katika maeneo mengine nje ya nchi.

Madhumuni hasa ya kuita mkutano huo uliohusisha pakubwa washikadau wote wanaohusika na maswala ya elimu yalikuwa ni kuona ya kwamba wanakuja na mbinu mpya ambayo ni jinsi ya kuendeleza masomo katika kiwango kingine cha juu zaidi.

Hata mkutano huo uliambatana vyema na matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa siku chache zilizopita.

Kutokana na matokeo hayo, MKU iko tayari kuwasajili wanafunzi waliopita vyema.

“Tunataka kuona ya kwamba chuo chetu kinaonekàna katika ramani ya ulimwengu kutokana na jinsi tunavyoendesha elimu yetu,” alifafanua Prof Gicharu.

Alipongeza bodi nzima pamoja na wahadhiri kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuleta matokeo mazuri katika chuo hicho.

“Nina furaha kusema ya kwamba mmeonyesha ujuzi wa hali ya juu na kukiweka chuo chetu mahali pa kuonekana ulimwenguni. Zidini kuongeza juhudi ili tupige hatua zaidi,” alisema Prof Gicharu.

Naye Naibu Chansela Prof Jaganyi aliwashukuru wahadhiri wote na wasimamizi kwa kufanya kazi kwa mwelekeo moja jambo lililofanya chuo hicho kutambulika na wengi.

“Katika siku zijazo tuna imani tutafanya bidii zaidi ili kuendeleza sifa za chuo hiki,” alieleza msomi huyo.

Alisema tangu mlipuko wa janga la Covid-19 mwaka wa 2020 chuo hicho kimepitia masaibu mengi lakini sasa wamejipanga vyema ambapo hata masomo yanaendeshwa kidijitali kupitia mtandao hata mwanafunzi akiwa sehemu za mbali.

Chuo cha MKU pia kimefungua vitengo zaidi kama vya udaktari, na sheria huku pia wakizingatia maswala ya kiufundi.

Alisema vitengo vyote vya masomo vitaimarishwa ili kila mwanafunzi apate haki yake ya kielimu.

Prof Jaganyi alisema chuo hicho kimetilia mkazo maswala ya teknolojia na utafiti ili kila mwanafunzi akikamilisha masomo yake awe na mwelekeo wa kubuni kazi kibinafsi bila kutegemea ajira kutoka kwa serikali.

Mkutano huo uliangazia mwongozo wa kutafuta mwelekeo mwafaka wa elimu kupitia kituo cha ODEL kuwafaa wanafunzi wanaosomea mtandaoni.
  • Tags

You can share this post!

Wanaraga wa KCB watolewa jasho wakipiga Strathmore Leos...

Magoha, msomi aliyejituma kwa yote aliyoyafanya

T L