Habari

Wahalifu, walanguzi mihadarati eneo la Mlima Kenya waonywa

August 30th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

HALI ya usalama katika eneo la Juja Farm, Kaunti ya Kiambu, imezorota huku pombe haramu na mihadarati ikipatikana Gatundu Kaskazini na Juja.

Kamishna wa eneo la Kati Bw Wilfred Nyagwanga amesema tayari maafisa wa usalama wameweka mikakati maalum ambapo kwa siku chache zijazo raia wataanza kuona mageuzi.

“Serikali haiwezi kushindwa kutekeleza wajibu wake. Wahalifu ambao wamechomoza vichwa vyao kuhangaisha wananchi watajilaumu wenyewe. Serikali huwa haizungumzi mengi kuhusu jinsi itakavyokabiliana na wahuni hao lakini mtaona majibu,” alisema Bw Nyagwanga.

Wakazi wa kijiji cha Juja Farm hivi majuzi walivamiwa na wahalifu usiku ambapo inadaiwa wakazi wengi walipokea kichapo kikali huku wakiporwa mali yao.

Wakati huo huo pia kumekuwa na tetesi kuwa pombe haramu ya changaa na ya kienyeji imerejea kwa fujo katika maeneo ya Kiambu na Gatanga.

Wananchi wamewasilisha malalamishi kwa serikali wakidai ya kwamba vijana wengi wamepoteza mwelekeo wakiacha majukumu mengi kufanywa na wakongwe.

“Hatutakubali kuona watu wenye tamaa ya kupata pesa wakiharibu vijana katika maeneo hayo. Wakati wowote kutoka sasa mtajionea jinsi serikali inavyokabiliana na watu kama hao,” alisema.

Alitoa amri maskani zote za kuuzia pombe zilizoko chini ya mita 300 kutoka kwa makazi ya watu zifungwe mara moja.

“Wale wote wanaouza pombe na hawana leseni wasiruhusiwe kuendelea na biashara hiyo. Iwapo yeyote atakiuka sheria hiyo baa yake ifungwe,” alisema kamishna huyo.

Alitoa onyo kali kwa machifu wote wafanye juhudi kuona ya kwamba wanaangamiza pombe haramu na mihadarati katika maeneo yao ama wapigwe kalamu mara moja.

“Iwapo hamtajikaza kumaliza janga hilo la pombe haramu na mihadarati katika maeneo yenu bila shaka mtapoteza krauni zenu,” alisema Bw Nyagwanga.

Alitoa amri pia watu wale wanaofanya kazi ya kupiga mawe kuyafanya kokoto eneo la Juja wachunguzwe kikamilifu kwa sababu maeneo hayo ni mapango wanakojificha wahalifu mchana halafu usiku wanatekeleza uovu wao.

Naye Naibu Gavana wa Kiambu Bw James Nyoro ambaye ndiye kaimu gavana wakati huu ambapo Ferdinand Waititu anakabiliwa na kesi , alisema tayari ameingia ofisini kwa kishindo kwani kazi lazima ifanywe kwa utaratibu ufaao.

Alisema kwa muda mrefu askari wa Kaunti ya Kiambu wamekuwa wakisumbua wafanyabiashara kwa kuwahangaisha bila sababu.

“Tayari nimekuja na mbinu ya kuwachuja na kutafuta maafisa walio na vyeti na tabia njema ili niweze kuweka mambo sawa,” alisema Bw Nyoro.

Alisema miradi yote iliyokosa kukamilika itafufuliwa ili ikamilike mara moja.

Alisema watatoa leseni kwa wauzaji pombe ambao wamefuata sheria zote zinazostahili.

“Hatutaki kubahatisha mambo kwani tunataka kila kitu kifanyike kwa njia ya haki bila minung’uniko ya kila mara. Kila mfanyakazi atafanya kazi katika mazingara mazuri,” alisema Bw Nyoro.

Alisema tayari wamekubaliana na serikali kuu ya kwamba askari wa kaunti ya Kiambu watafanya kazi kwa ushirikiano na wale wa serikali kuu ili kuwe na uwazi katika utendaji kazi.