Wahalifu wavuruga shughuli za kupata riziki vijijini Lamu

Wahalifu wavuruga shughuli za kupata riziki vijijini Lamu

NA KALUME KAZUNGU

UTOVU wa usalama unaoshuhudiwa Lamu umeathiri shughuli za kiuchumi wachimba migodi na wahudumu wa bodaboda wakisitisha biashara zao kwa kuhofia kushambuliwa.

Kwenye migodi ya Kiongwe-Timboni, tarafa ya Mpeketoni ambako zaidi ya familia 2,000 hutegemea uchimbaji wa mawe kwenye machimbo hayo, wachimba mawe wamekosekana kwenye sehemu zao za kazi.

Mmoja wao, Bw Kamau Wamwangi, alisema tangu mauaji kushuhudiwa Januari 2, 2022, yeye binafsi hajakanyaga timboni kuendeleza shughuli zake kwa kuhofia kulengwa na wavamizi.

Bw Wamwangi alisema wenzake wengine pia wamelazimika kufanya vibarua mbadala mitaani kwani mauaji yanayoshuhudiwa vijijini yamewatia hofu.

“Tegemeo letu pekee kukimu familia zetu ni kuchimba mawe ya kujengea. Timbo zetu nyingi ziko sehemu za vichakani ambazo zimekuwa zikilengwa na magaidi. Tangu mauaji yaanze kutekelezwa eneo hili, sijakanyaga tena kwenye migodi. Tunaumia,” akasema Bw Wamwangi.

Anasema tangu kafyu ilipowekwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i wiki jana, yeye hulazimika kufika kazini kuchelewa na kufunga kazi mapema ili kuepuka kujipata nje masaa ya kafyu.

Baba huyo wa watoto watano anasema kutokana na kuathirika kwa kazi yake, amekuwa hawezi kulipa karo ya baadhi ya watoto wake walioko shule za sekondari na vyuoni.

Wakati huo huo, karibu familia 300 zimepiga kambi kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu baada ya kutoroka vijijini kwa sababu ya utovu wa usalama ambao umekuwa ukishuhudiwa katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita.

Familia 250 zimepiga kambi katika shule ya kibinafsi ya Shalom Academy, mjini Kibaoni huku zaidi ya 50 zikiishi katika shule ya Msingi ya Juhudi.

Waliotoroka walikuwa kwenye vijiji vya Widho, Juhudi, Marafa, Muhamarani, Salama, Mashogoni ambako watu 13 wakiwemo maafisa wa usalama waliuawa.

Simon Gatete, ambaye ni mkimbizi katika Shalom Academy, alisema licha ya maisha kuwa magumu kambini, yeye na familia yake wataendelea kuishi pale kwani kambi hiyo imepakana na kituo cha polisi cha Kibaoni.

Mary Wambugu, mkazi wa Mashogoni, aliitaja kuwa bahati kwamba yupo salama kambini baada ya kijiji chao kuvamiwa na magaidi Jumanne asubuhi, ambapo walichoma nyumba kadhaa kabla ya kuchinja mbuzi na kubeba nyama na kutorokea msituni.

Diwani wa Wadi ya Mkunumbi, Paul Kimani, aliisihi serikali ihakikishe vituo vya polisi na jeshi vinabuniwa kwenye maeneo yote ya mashambani ili kuzuia uvamizi.

You can share this post!

KIMANI NJUGUNA: Wakenya wajifunze na kuchagua viongozi...

Korti yazima hela za kaunti

T L