Habari MsetoSiasa

Wahandisi wamlilia Raila kampuni za kigeni kupewa kandarasi zao

March 6th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

MUUNGANO wa Wahandisi Nchini (IEK) Jumanne ulielezea changamoto zinazokumba taaluma hiyo kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, ikiwemo hali ya kampuni za kigeni kupewa kandarasi za miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Wahandisi hao walilalamika kuwa serikali imekuwa ikipeana kandarasi za miradi yake kwa kampuni za nje ilhali wataalamu wa humu nchini wanaachiwa miradi midogo ama kukosa kabisa, wakiomba watengewe asilimia 40 ya miradi ya ujenzi na ushauri nchini.

“Tumebaini kuwa sekta hii inatawaliwa na kampuni kubwa za kigeni haswa katika miradi mikubwa, huku wanakandarasi wa humu nchini wakiachwa nje,” ujumbe waliomfikishia Bw Odinga katika afisi yake ya Capitol Hill, Jjiji Nairobi ukasema.

Wahandisi hao pia walisema, wanataka Idara ya Uhamiaji kushirikiana na Bodi ya Wahandisi Nchini iwe inafahamu nafasi zilizopo kabla ya kutoa idhini kwa wahandisi wa kigeni kufanya kazi nchini.

“Tunataka wahandisi wetu washiriki katika usimamizi wa sekta hii panapofaa,” akasema naibu mwenyekiti wa IEK, Bi Jane Mutulili.

Waliendelea kusema kuwa hali ya kutoa kandarasi kwa wahandisi wa kigeni imesababisha kampuni zisizoweza kazi kupewa miradi muhimu kwa taifa, ujumbe wao ukirejelea sakata zinazoendelea za mabwawa na ununuzi wa treni kuukuu na Shirika la Kenya Railways.

Wahandisi hao aidha, walilalamika kuwa katika muongo mmoja uliopita, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya uhandisi imekuwa ikipungua, huku hali ya vyuo vya mafunzo anuwai kugeuzwa kuwa vyuo vikuu ikifanya idadi ya wanafunzi wanaopokea mafunzo ya kiufundi ikupungua.

IEK vile vile ilipendekezea serikali kuacha kuuza mafuta yanayochimbwa Turkana bila kuyasafisha kufikia kiwango cha kutumika, ikisema serikali ikiwekeza kuyasafisha itakuza viwanda vitakavyotoa ajira kwa watu wengi.

Wahandisi hao walikuwa wamemtembelea Bw Odinga kwa heshima yake kama Balozi wa Muungano wa Afrika (AU) katika sekta ya Miundomsingi.

Ziara hiyo kwa Bw Odinga ilikuwa moja tu kati ya nyingi ambazo mashirika mbalimbali pamoja na viongozi wamekuwa wakifanya kwa Bw Odinga tangu muafaka wa Machi 9, 2018 na kuteuliwa kwake kuwa balozi wa Miundomsingi barani mwaka uliopita.

Jumatatu, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri alifika katika afisi ya Bw Odinga kumfahamisha na kushauriana naye kuhusu utendakazi wa jopokazi lililoundwa kusuluhisha matatizo katika sekta ya miwa.

Bw Kiunjuri alikuwa pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo na maafisa wa wizara.

Takriban wiki mbili zilizopita, kiongozi huyo alitembelewa na waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, pamoja na viongozi wengine mashuhuri kujadiliana kuhusu mikakati ya uandalizi wa kongamano la miji ya Afrika litakaloandaliwa Jijini Kisumu mnamo 2021, maarufu kama Africities.

Hii ni kando na ziara aliyofanya kwa afisi ya Bw Odinga Capitol Hill, Rais mpya wa Nchi ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Felix Tshisekedi, majuzi alipokuwa humu nchini kwa ziara rasmi.