Habari Mseto

Baadhi ya wahanga wa mafuriko Mukuru-Kaiyaba wakosekana orodha ya kupokea Sh10,000

June 9th, 2024 3 min read

SAMMY KIMATU NA NYABOGA KIAGE

MAKUMI ya waathiriwa wa mafuriko katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba jijini Nairobi ni miongoni mwa watu ambao majina yao hayapo kwenye orodha iliyowasilishwa kwa ofisi ya mkuu wa tarafa South B, kwa malipo ya Sh10,000.

Malipo hayo yatatolewa kwa kila mwathiriwa kutoka kwa Hazina ya Serikali kwa walioathiriwa na mafuriko maeneo ya mkondo wa Mto Ngong.

Waliozungumza na Taifa Leo bila kutajwa majina walidai kuwepo kwa udanganyifu katika mchakato mzima kuanzia kuwasilisha majina yao hadi ngazi ya malipo.

Katika kisa kimoja, wale ambao nyumba zao zilisombwa na maji kwanza kwa kuwa karibu na Mto Ngong hawamo katika orodha ya majina yaliyowasilishwa kwa ofisi ya Kamishna Msaidizi eneo la South B.

Akizungumza Jumapili, naibu kamishna wa kaunti ya Starehe, Bw John Kisang aliagiza majina yaliyokosekana ya waathiriwa halisi yawasilishwe kwa afisi ya South B na nakala yao kuwasilishwa kwake.

“Hatuwezi kuruhusu njia zisizo za kawaida kufanywa katika ofisi ya serikali. Tutathibitisha ili kuangalia hitilafu hizo lakini tukipata mtu alihusika katika ufisadi, atawajibika,” Bw Kisang alisema.

Serikali ilikuwa imeahidi kutoa Sh10,000 kwa kila mwathiriwa wa mafuriko kabla ya zoezi la kuwahamisha kuanzishwa ili kuondoa majengo yaliyoko kwenye kingo za Mto Nairobi, Mto Ngong na Mto Mathare jijini Nairobi.

Huku hayo yakijiri, maswali sasa yanaibuliwa kuhusu maandamano yanayoendelea Mathare ndani ya Kaunti ya Nairobi huku baadhi ya wenyeji wakisema wanalazimishwa kutoa hongo ili nyumba zao zisibomolewe.

Mwishoni mwa juma, maafisa kutoka Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) walizuru eneo ambako nyumba zinabomolewa na kusema kuwa Watu Wanaoishi na Ulemavu (PWD) walikuwa wakitelekezwa.

Bw Cornelius Oduor ambaye ni Naibu mkurugenzi mkuu wa KHRC alisema kuwa Sh10,000 ambazo Rais William Ruto aliahidi zitatolewa kwa wale ambao wataathiriwa na ubomoaji huo zilikuwa zikienda mikononi mwa watu wasiofaa.

“Kuna ukosefu wa uwazi katika utoaji wa fedha na hata misaada ambayo inakusudiwa kwa walioathirika haifikii mikononi mwa watu wenye ulemavu,” alisema.

Aliiomba serikali kuwajali wanawake na watoto pia kwa kuhakikisha wanapata msaada unaostahili.

Bw Oduor alisema kuwa watu wengi kwa sasa hawana makao kutokana na ubomozi unoendelea.

“Tunapozungumza sasa hivi, familia nyingi sasa zimepiga kambi ndani ya vitongoji duni vya Mathare kwani hawana mahali pa kwenda. Familia kadhaa hazina makao baada ya nyumba zao kubomolewa,” akasema Bw Oduor.

Bw Patrick Taware ambaye ni kiongozi wa watu wanaoishi na ulemavu ndani ya wadi ya Huruma, Mathare alisema kuwa orodha hiyo ambayo ilitolewa kwa walengwa wa pesa walizoahidiwa na serikali haikuwahusisha.

Alishangaa kwa nini Rais Ruto aliyeahidi kuisimamia serikali kupuuzilia mbali ahadi zake.

“Pesa ambazo zilikusudiwa kutolewa kwa wale walioathirika zilikuwa zikienda kwa mikono isiyofaa. Rais alisema anataka kufanya kazi na wapiga kura ambao ni pamoja na sisi, kwa nini sasa anavunja ahadi yake?” Bw Taware akauliza.

Wakiwa bado katika eneo hilo hilo, uongozi wa shule ya kimataifa iitwayo Still I Rise ulimshutumu chifu wa eneo hilo kwa kuomba rushwa ili kukomesha ubomoaji wa taasisi hiyo.

Bi Susan Irungu ambaye ni mkurugenzi wa shule aliambia Taifa Leo kwamba alifikiwa na ujumbe ambao uliongozwa na chifu wa eneo hilo ambao ulienda mbele na kudai hongo ili kukomesha ubomoaji katika taasisi hiyo.

“Walitaka kubomoa jengo hili la orofa mbili linalohifadhi maofisi na madarasa. Ujumbe ulidai niwape Sh1 milioni jambo ambalo nilipinga,” Bi Irungu alisema.

Alishangaa ni kwa nini maafisa hao walikuwa wakiitisha mlungula ili kuokoa mali hiyo ambayo inadaiwa kuwa kwenye eneo la mkondo wa maji katika Mto Mathare.

Alisema kuwa hakuna afisa wa serikali ambaye alikuwa amewatembelea na kutoa notisi kwamba wanapanga kubomoa jengo hilo.

Bw Nocolo Govoni ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji aliambia Taifa Leo kwamba anashangaa ni kwa nini kulikuwa na mipango ya kubomoa shule hiyo ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa miaka mitano.

Mkurugenzi Mtendaji wa shule hiyo, Nicolo Govoni, anasema wanachotaka ni kuambiwa na serikali kwa nini imewachukua miaka yote kufikia uamuzi kwamba shule yao iko kwenye ardhi iliyo katika mkondo wa maji,

Bw Govoni alisema kuwa taasisi hiyo ilipokea cheti cha utendakazi hivi majuzi kutoka kwa Wizara ya Elimu.

Aidha, alisema kuwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) ilitembelea kituo hicho kufanya utathmini na ukaguzi kabla ya kuwapa cheti cha kuwa mahali hapo.

“Tumepokea leseni ya kuwa na shule kwa miaka mitano ijayo. Walifanya ukaguzi wa majengo yote miezi miwili iliyopita. Kwa nini walitupatia cheti ikiwa tuko kwenye ardhi ya mto?” akashangaa.

Bi Phillis Muhonja ambaye ni chifu wa Mathare na anayedaiwa kudai hongo alikana madai hayo. Kulingana naye, alisema hata hakujua jambo hilo.

“Ninachojua ni kwamba wanafunzi waliandamana lakini sifahamu madai kwamba niliitisha hongo,” alisema.

Zoezi la ubomoaji lilianza kufuatia agizo la Rais Ruto kwamba majengo yote yaliyo kwenye eneo la ukingo wa maji yaondolewe.

Rais Ruto pia alisema majengo ambayo yamejengwa mita 30 kutoka mito pia yanapaswa kubomolewa.