Kimataifa

Wahindi wakejeli utumizi wa mafuta ya ng'ombe kutengeneza pesa

January 23rd, 2019 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

JAMII ya Hindu inaitaka benki ya Reserve kutoka Australia kuanza kuchapisha sarafu za noti zisizoundwa kutumia sehemu za wanyama, baada ya kubainika kuwa mafuta ya ng’ombe hutumika kuzichapisha.

Noti mpya ambazo zimeundwa na tayari kuanza kutumiwa katika nchi hiyo, sarafu za noti za $5, $10 na $50. Sarafu za $20 na $100 zitaanza kutumiwa 2019 na 2020 mtawalia.

Wiki hii, Rais wa jamii ya Kihindi duniani Rajan Zed aliitaka benki ya RBA “kuonyesha heshima kwa hisia za Wahindi na kutengeneza noti zisizotumia nyama ya ng’ombe kama kiungo cha kutengeneza.”

Kiwango kidogo cha ‘tallow’, ambayo hupatikana kutoka kwa mafuta ya nyama ya mbuzi ama ng’ombe, kinatumika kutengenezea sarafu hizo ili kuzipa ubora fulani.

Hata hivyo, ng’ombe ni myama takatifu katika dini ya Kihindi na ulaji wake unakinzana na imani zao. Aidha, umepigwa marufuku huko.

Bw Zed sasa anamtaka gavana wa RBA Philip Lowe kuchukulia suala hilo kwa uzito na kurekebisha.

“RBA ingekuwa na busara na kusoma vya kutosha kufahamu mahitaji ya kidini ya wateja wake kabla ya kuwekeza kiwango kikubwa cha pesa hivyo kutengeneza sarafu hizo,” akasema.

Watu wasiokula nyama aidha wameeleza ghadhabu zao kuhusiana na suala hilo.

Ufichuzi kuwa ‘tallow’ hutumiwa katika utengenezaji wa noti ulitolewa Novemba 2016 wakati benki ya Uingereza ilikiri kwenye twitter kuwa kuna kiwango kidogo chake kinachotumika.

Kupitia ujumbe, kampuni hiyo ilisema kuwa inajaribu kukoma kutumia bidhaa hiyo, japo ikisema kuwa “lakini ni hatua ngumu sana.”

Hii si mara ya kwanza kwa kiungo hicho kwenye sarafu kusababisha mzozo, kwani mnamo 2002 ilibainika kuwa kampuni ya vyakula McDonald’s ilikuwa ikitumia tallow kupika chakula cha French Fries. Hata hivyo, baadaye, kampuni hiyo ilianza kutumia mafuta ya nafaka na mimea mingine.

Kuna zaidi ya Wahindi 440,000 nchini Australia kulingana na sense iliyotekelezwa mnamo 2016 na dini hiyo ni ya nne kwa wingi wa wafuasi, baada ya zile za Kikristo, Kiislamu na Wabuddha.