Habari Mseto

Wahisani waagizwa kutii kanuni za KCPE wakitoa mlo

October 8th, 2018 2 min read

Na HAMISI NGOWA

SERIKALI imewataka wahisani wanaopanga kutoa misaada ya chakula kwa watahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) kuhakikisha wanaandaa mipango hiyo mapema, ikisema haitaruhusu maandalizi kufanyika wakati ambapo mitihani itakuwa ikiendelea.

Mkurugenzi wa Elimu katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, Bw Newton Okwatsa aliwataka wahisani wote ambao huwapelekea watoto vyakula wakati wa mitihani kuhakikisha wanafuata utaratibu ulioko ili wasiathiri mitihani hiyo kwa njia yoyote,

Alisema hatua hiyo ni mojawapo ya mikakati ya kuhakikisha hakuna visa vya wizi wa mitihani au udanganyifu vinavyoshuhudiwa katika miaka iliyopita.

Kulingana na Bw Okwatsa, japo ni jambo la kutia moyo kwa wahisani kujitokeza na kuwasaidia watahiniwa kwa chakula wakati wa mtihani huo,ni muhimu kutilia maanani maslahi ya watahiniwa wakati huo.

“Sio kwamba tunawakataza watu kuwasaidia watahiniwa kwa chakuala, lakini tunasisitiza kwamba zoezi hilo ni lazima lifanyike kulingana na utaratibu ulioko tena mapema,’’ akasisitiza.

Alisema wale walio na nia ya kuwasaidia watahiniwa hao kwa chakula, wanaweza kushirikiana na walimu wakuu wa shule na kupanga jinsi ambayo wataweza kutoa misaada yao kwa watahiniwa hao.

Hatua ya kuwapelekea wanafunzi wanaotahinwa chakula cha mchana imekuwa likifanyika katika shule nyingi nchini ambapo viongozi pamoja na watu binafsi hujitolea kwa kuwanunulia wanafunzi chakula cha mchana.

Hatua hiyo huwasaidia wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali na shule wanayofanyia mtihani huo, kuokoa wakati wanaotumia wakitembea kuelekea makwao kwa minajili ya kupata chakula cha mchana.

Kando na kuokoa muda kwa wanafunzi, pia huwasaidia wanafunzi kutoka familia maskini ambao hawana uwezo wa kupata chakula cha mchana hata wanaporudi nyumbani.

Hata hivyo, hatua hiyo ilipigwa marufuku na aliyekuwa Mshirikishi Mkuu wa Serikali ya kitaifa Ukanda wa Pwani, Bw Nelson Marwa wakati wa kukaribia kwa kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2017.

Lakini haikuweza kubainika kwa nini Bw Marwa aliamua kuzima zoezi hilo au kutaka lifanywe kwa taratibu zinazofaa tofauti na lilivyokuwa likifanywa na baadhi ya wanasiasa ambapo baadhi yao walikuwa wakipachika karatasi zenye majina yao kwenye vifaa vya kufungia chakula au hata kwenye chupa za maji ya kunywa.