Habari

Wahitimu TIBS Thika wahimizwa wawe wabunifu na wenye kujiamini

September 20th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwa na subira na kujituma kwa kujitegemea baada ya kufuzu elimu ya chuoni.

Mwanzilishi na pia Mkurugenzi wa chuo cha Thika Institute of Business Studies (TIBS), Bw James Kamau, amewashauri wahitimu wa chuo hicho kuwa na maono baada ya kufuzu katika masomo yao.

Amesema masomo ya kuhitimu peke yake hayawezi yakamfanya mtu kuwa mkamilifu maishani, lakini pia maadili mema na uvumilivu ni muhimu katika maisha.

“Ninawashauri nyinyi wahitimu 800 mliopita mitihani yenu kuwa sasa ndio mtaanza mkondo wa maisha. Hayo yote inahitaji mtu mwenye subira, mnyenyekevu, na aliye tayari kujituma,” amesema Bw Kamau.

Aidha ameeleza kwamba maisha sio kitu cha kufanyia mzaha bali ni mtihani wa kila mara ili mtu aweze kufanikiwa.

Baadhi ya wahitimu wa Thika Institute of Business Studies (TIBS). Wanafunzi wapatao 800 wamefuzu Septemba 20, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliongeza kuwa ni sharti kila mmoja awe na maono katika maisha ili kufanikisha malengo yake.

“Mkiingia katika ulimwengu wenye changamoto na majaribu mengi, ninawahimiza muwe mabalozi wazuri na kuhakikisha mnainua nyota ya chuo chenu juu. Hiyo pekee itakuweka katika mwelekeo mwema,” alisema Bw Kamau.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina ambaye amehudhuria hafla hiyo Ijumaa amewahimiza wahitimu hao kuwa mstari wa mbele kubuni ajira kwa kufuata ajenda nne muhimu za serikali.

“Ulimwengu wa sasa ni wa nafasi chache za ajira kutoka kwa serikali na kwa hivyo nyinyi vijana mliokamilisha masomo yenu ni sharti mjiamini kwa kujiunga pamoja ili kujiajiri wenyewe,” alisema Bw Wainaina.

Kuboresha uchumi

Amewashauri wahitimu hao waliofuzu wa TIBS kutumia ujuzi wao kubuni ajira ili kuboresha uchumi wa nchi.

Amesema aghalabu kila mtu huanzia chini akija juu na huo ndiyo mwelekeo unaostahili katika maisha.

Hakuna haja ya kutamani kufika kileleni kwa haraka.

Amesema tayari ofisi yake imetenga takribani Sh4 milioni zitakazotumika kuwainua wanafunzi walio chuoni na hawajiwezi kwa kulipa karo.

“Hata ingawa sio kiasi kikubwa cha fedha, lakini kila mwanfunzi hata akipata kitu kidogo itakuwa nafuu kwa mzazi mwenyewe,” amesema Bw Wainaina.

Mgeni wa heshima katika hafla hiyo Profesa Wangari Mwai ambaye ni Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha USIU jijini Nairobi, amesema wahitimu wote waliopata shahada ya diploma na cheti cha kuhitimu wanastahili kuwa na nidhamu wakati wote wakiwa katika ulimwengu wa majaribio.

“Ni lazima mjizatiti muwe watu wenye maadili mema na wanaoweza kuaminika katika jamii.Pia ni vyema kujijulisha na maisha ya vijijini badala ya kukimbilia mijini kwa dhana ya kupata kazi nzuri,” amesema Prof Mwai.

Amewahimiza kuwa wavumilivu na kujiamini wakati wote wanapofanya jambo lolote lile.

Bw Patrick Ngotho ambaye pia ni mmoja wa wakurugenzi katika chuo hicho, amewashauri wahitimu kushirikiana kila mara na washindi ili kufanikiwa katika maisha.

“Kila mmoja ni sharti awe na maisha yake kivyake bila kuigiza ya mwingine. Ni vyema kuwa na maono na usikate tamaa katika maisha,” ameshauri Bw Ngotho.