Habari Mseto

Wahitimu wa Zetech wahimizwa kuwa wabunifu

November 19th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAHITIMU wa Chuo Kikuu cha Zetech mjini Ruiru, wamehimizwa kujizatiti na kukabiliana na maisha kwa kubuni kazi wenyewe.

Mgeni wa heshima katika hafla hiyo, mkurugenzi wa benki ya Standard Chartered Bw Kariuki Ngari, aliwahimiza wahitimu hao kuwa makini wanapoingia katika ulimwengu wa ushindani mkali.

“Ulimwengu huu unahitaji mtu anayejiamini na kujitolea kufanya jambo kwa makini akijua ya kwamba kuna ushindani kutoka kila pembe. Kwa hivyo, nawahimiza muwe na maono kwa kujiamini kwa lolote mnalofanya,” alisema Bw Ngari.

Alisema wahitimu hao watastahili kuwa na mvutio kwa kila jambo watakalofanya ili wawe ni jawabu kwa maswala muhimu watakayotekeleza.

Alitoa changamoto kwa kusema ya kwamba kupata utajiri ni kufanya bidii kutoka chini wala sio kwa kuyafanya mambo kwa pupa.

Alisema ni sharti ufanye bidii kwa vyovyote vile.

“Huwezi kutajirika kwa miezi michache; ni sharti ufanye bidii na unyenyekee kwa kuwa mtu mwenye utu,” alisema Bw Ngari.

Mwelekeo mpya

Chansela mkuu Profesa Njenga Munene alisema ni muhimu kuegemea katika mwelekeo wa mtandao wa Intaneti kwa sababu huo ndiyo mwelekeo wa kizazi cha kisasa.

Wahitimu hao walipokea shahada za digrii na vyeti vya diploma katika masomo tofauti kwenye vitengo na taaluma tofauti.

Aliwahimiza wahitimu wote kufanya juhudi kuona ya kwamba wanapotoka nje katika ulimwengu wa ushindani, wanakuwa na mwelekeo wa kuwafaa na wasikubali kuingia kwenye majaribu ya uovu.

“Wakati huu kuna majaribio mengi na kwa hivyo kila mmoja lazima awe makini na ajue ni nani aliye rafiki wa haki na wa kupotosha,” alisema Prof Munene.

Profesa Susan Alfano Nkinyangi aliwapongeza wahitimu kwa juhudi kubwa waliofanya ya kukamilisha masomo yao.

“Kwa hivyo iliyobaki sasa ni kuona ya kwamba unafanya bidii katika maswala yote unayokumbana nayo maishani,” alisema Profesa Nkinyangi.

Mbunge wa eneo la Maara Bw Kareke Mbiuki alisema atapeleka mswada bungeni utakaowasaidia wanafunzi wote waliokamilisha elimu ya chuo kikuu kupata nafasi ya kuingia kwenye mtandao kwa uwazi ili kufanya utafiti wao kwa urahisi wakijiendeleza katika kiwango cha juu masomoni.

“Tunaelewa wazi kuwa teknolojia ya kisasa ndiyo njia ya kipekee ya kupata jawabu kwa kila jambo linalohitajika na kwa hivyo mtandao utakuwa ni njia ya pekee ya kujiendeleza zaidi,” alisema Bw Mbiuki.