Habari Mseto

Waholanzi sasa ndio wateja wakuu wa bidhaa za Kenya

March 28th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

TAIFA la Uholanzi limekuwa mwagizaji wa pili mkubwa zaidi ya bidhaa za Kenya, kwa kuipiku Uganda ambayo awali ilikuwa ikinunua zaidi bidhaa za Kenya kote ulimwenguni.

Bidhaa zilizonunuliwa na wafanyibiashara wa Uganda zilipungua kwa karibu Sh1 bilioni Januari, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Hii ina maana kuwa bidhaa zilizouzwa na Wakenya nchini Uganda zilipungua kwa asilimia 21.8, hadi Sh3.52 bilioni, kulingana na takwimu za hivi punde za Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS).

Uganda imo katika ni nambari ya tatu katika orodha ya mataifa yaliyonunua bidhaa za pesa nyingi zaidi kutoka Kenya.

Hii ni baada ya kuondolewa katika nafasi ya mwanzo na Pakistan mwishoni mwa mwaka jana, na sasa Uholanzi.

Bidhaa ambazo huagizwa zaidi kutoka Kenya na Uholanzi ni maua. Biashara hiyo iliongezeka kwa asilimia 10.38 hadi Sh4.19 bilioni Januari.

Pakistan iliipa Kenya Sh7.31 bilioni kutokana na mauzo ya majani chai. Hata hivyo, mapato hayo yalipungua kwa asilimia 0.02.