Habari Mseto

Wahu kizimbani kwa kuzuia magari Kileleshwa

November 22nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSANII wa nyimbo za dini alishtakiwa Alhamisi katika mahakama ya Milimani kwa kuzuia magari mengine barabarani.

Bi Rosemary Wahu alikanusha mashtaka matatu aliposhtakiwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Bi Elector Riany.

Mashtaka dhidi ya Wahu yalikuwa mnamo Novemba 21 mwendo wa saa nne katika barabara ya Ring Road iliyoko mtaani Kileleshwa, aliendesha gari lake muundo wa Mercedez Benz 440 kwa njia ya hatari.

Alishtakiwa pia aliiendesha bila leseni.

Mahakama ilifahamishwa mwimbaji huyu wa nyimbo za kumsifu Mungu alikuwa anayapita magari kwa kasi na kwa njia ya hatari.

Pia alishtakiwa kuyatatiza magari mengine kwa kuyazuia na kusababisha msongamano.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Upande wa mashtaka haukupinga ombi hilo na mahakama ikamwachilia kwa dhamana ya Sh15,000.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili upande wa mashtaka ueleze iwapo umemkabidhi nakala za ushahidi.