Makala

Wahubiri kizazi kipya wawatoa jasho mapasta wazoefu

February 4th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA muda mrefu, tasnia ya uhubiri katika eneo la Mlima Kenya ilidhibitiwa na mapasta wawili maarufu, waliokuwa na ufuasi mkubwa kotekote.

Walikuwa na vipindi kwenye redio na runinga, hali iliyoimarisha ufuasi wao hata nje wa eneo hilo.

Ni jambo lililowafanya kuwa na umaarufu unaolingana na ule wa wanasiasa.

Wawili hao ni Askofu JJ Gitahi wa Kanisa la Priesthood na mwenzake Paul Kuria wa kanisa la Joy Centre. Makanisa hayo yote yako jijini Nairobi.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, ni vituo vya redio vya Kameme, Inooro, Coro, na Radio Citizen vilivyovuma katika eneo hilo.

Wahubiri hao walishiriki kwenye vipindi vyote vya mahuburi na kutoa ushauri kwa jamii, ikizingatiwa huo ndio wakati ambapo vituo hivyo vilikuwa vimeanza kupenya katika maeneo ya mashambani.

Kwa karibu miaka 20—kati ya 2000 na 2020—wao ndio walikuwa wahubiri wenye umaarufu, wenye ufuasi mkubwa wa maelfu ya watu.

Hata hivyo, umaarufu wao ulianza kutikisika mwaka 2023, kufuatia ujio wa kizazi kipya cha wahubiri katika eneo hilo, kinachoonekana kuwavutia vijana zaidi kuliko wawili hao.

Wimbi hilo la wahubiri hao wa kisasa linaonekana kuvumishwa na mcheshi Benson Gathungu (maarufu kama Muthee Kiengei), aliyeanzisha kanisa lake la Jesus Christ Compassion Ministries (JCM) lililo katika eneo la By-Pass, Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Ijapokuwa kanisa hilo lilianzishwa karibu miezi minane iliyopita, umaarufu wake unaonekana kusambaa kwa kasi sana.

Kwa muda huo, limefanikiwa kufungua matawi mengine katika maeneo kama Nyahururu, Nakuru, Embu, Nyeri, na Murang’a.

Umaarufu huo unaonekana kuwashawishi watu wengi kuyaacha makanisa yao ya zamani na “kuabiri garimoshi la Muthee Kiengei” ambaye wakati anapohuburi, huwa anajiita ‘Kaasisi Ben’.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya burudani katika ukanda huo, mafanikio hayo makubwa ndiyo yamewafanya baadhi ya wanamuziki maarufu wa nyimbo za injili kama Sammy Irungu, kutangaza azma ya kuanza makanisa yao binafsi.

“Kinachodhihirika ni watu wengi maarufu wameona kwamba kuna mafanikio na ufanisi mkubwa wa kifedha na umaarufu katika kuanzisha makanisa. Hilo ndilo bila shaka limewapa msukumo ‘macelebs’ katika eneo la Kati kuanza kutumia umaarufu wao kuanzisha makanisa,” asema Bw John Muchiri, ambaye ni mdadisi wa masuala ya burudani.

Kutokana na wimbi hilo jipya, kumeibuka migongano na vita vikali baina ya wahubiri wa hapo awali na wake wa kizazi kipya, kwani wanaonekana “kuwanyang’anya wafuasi wao”.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na makabiliano baridi baina ya Bw Kiengei na Askofu JJ, wafuasi wao wakitaja hilo kama vita vya kupigania umaarufu na udhibiti wa washirika wao.

Tofauti zao zilidhihirika mwishoni mwa mwaka 2023 kwenye mazishi ya mwanamuziki Muhiko Nebstar, wakati Askofu JJ alionekana kumkosoa Bw Kiengei kwa kuanza zoezi la kuwapa chakula washirika maskini katika kanisa lake.

“Huwezi kuwatosheleza watu kwa kuwapa chakula. Watu wana shida nyingi,” akasema JJ.

Hata hivyo, aijitetea kwa kusema kuwa alifasiriwa vibaya.

Baadaye, Askofu Kuria aliingilia ‘vita’ hivyo, akisema kuwa wahubiri wote wanafaa kuheshimiana bila kuzozana wala kuvutana kwa njia yoyote ile.

“Tunafaa kuheshimiana kwani mwito wetu mkuu ni kueneza injili kwa wafuasi wetu. Vita havitakupeleka popote,” akasema Bw Kuria.

Ijapokuwa wawili hao—Askofu JJ na Bw Kiengei—walitangaza kumaliza ‘vita’ vyao, wadadisi wanasema kuwa hilo linaonyesha mvutano uliopo baina ya wahubiri hao kutokana na mchipuko wa mapasta ‘celebs’ na uenezaji injili ya kisasa.