Wahubiri waelezea hofu yao kuhusu taharuki ya kisiasa

Wahubiri waelezea hofu yao kuhusu taharuki ya kisiasa

Na Joseph Openda

BAADHI ya viongozi wa kidini katika Kaunti ya Nakuru wameelezea wasiwasi wao kufuatia kile walichosema ni ongezeko la taharuki ya kisiasa nchini.

Viongozi hao kutoka madhehebu mbalimbali wameonya kuwa ongezeko la visa vya ghasia za kisiasa ni dalili za matukio mabaya ambayo huenda yakaikumba nchi katika siku zijazo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Mapasta katika kaunti hiyo, Pasta Alex Maina, waliziomba idara husika za serikali kuchukua hatua za haraka kuwakabili wanasiasa wote ambao wametajwa kuzichochea jamii zao.

Alikashifu visa vya hivi majuzi ambapo baadhi ya viongozi walihusishwa na madai ya kufadhili ghasia katika mikutano ya kisiasa, huku wengine wakishambuliana hadharani.

“Matukio yanayoshuhudiwa nchini ni dalili ya mikosi ambayo huenda ikatuandama. Kama viongozi wa kidini, tunataka kukashifu vitendo hivyo na kuziomba idara husika kuwakabili vikali wale wote ambao wametajwa,” akasema Pasta Ndegwa.

Viongozi hao waliunga mkono hatua ya Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kuwataja wanasiasa ambao nyendo zao zinafaa kutathminiwa.

You can share this post!

TZ yapuuza madai hospitali zimelemewa na wagonjwa wa corona

ICC yampata aliyekuwa kiongozi wa LRM na hatia