Makala

Wahubiri walia waliofungiwa riziki kwa baa kufungwa huingia kanisani bila sadaka

March 9th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

WACHUNGAJI katika eneo la Mlima Kenya sasa wanalalamika kwamba vita vinavyoendelea dhidi ya baa na walevi, vinaathiri huduma ya Mungu kwa kuwa ufisadi unaoandamana na harakati hizo unachuna hata sadaka za kanisa.

Askofu Simon Kinyanjui ambaye huongoza muungano wa makanisa ya kiasili eneobunge la Kangema, aliambia Taifa Leo kwamba baa zikifungwa, riziki nyingine nyingi hutatizika.

Alidai wachuuzi, wasanii, wahudumu wa biashara ya chakula na pia wafanyakazi ndani ya baa hukosa riziki.

Askofu Simon Kinyanjui. PICHA | MWANGI MUIRURI

“Waathiriwa wa kufungiwa riziki zao hufika kanisani bila hata sadaka,” akadai Bw Kinyanjui.

Naye mwenyekiti wa makanisa ya kiasili ya Mlima Kenya Askofu Edward Nyutu alisema Alhamisi kwamba serikali imelemewa na kutofautisha kati ya biashara na maadili ya kibiashara ambapo inaamrisha baa zifungwe kwa msingi wa maadili potovu ndani ya sekta.

“Maadili ni ya kumulikwa kisera huku mwekezaji binafsi akiandamwa kwa makosa yake mwenyewe. Hatua ya kutangaza kwamba biashara za watu zifungwe pasipo hata hukumu mahakamani haina maana,” akasema Bw Nyutu.

“Unaposikia mwekezaji amepoteza shehena ya Sh4.5 milioni mikononi mwa wanasiasa na magenge kama ilivyofanyika hivi majuzi katika Kaunti ya Nyeri moyo unasononeka kwa kuwa mabishano hadi sasa ni kwamba uharibifu wa mali hiyo ulichochewa na masilahi mengine wala si ya kisheria,” akaongeza.

Katika kisa hicho, Mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga wakiandamana na wafuasi wao, walivamia stoo za serikali katika makao makuu ya Mathira Mashariki na wakaharibu chupa 34,000 za pombe ya kampuni ya Patiala.

Mbunge wa Mathira Eric wa Mumbi abeba pombe aliyodai ni haramu akielekea katika eneo la kuiharibia nje ya stoo ya serikali iliyoko Mathira Mashariki. PICHA | MWANGI MUIRURI

Hadi sasa, jopo la mahakama kuhusu ukadiriaji ubora wa bidhaa limetoa uamuzi kwamba uharibifu huo haukuzingatia mkondo wa kisheria kwa kuwa wanasiasa hao hawakuwa na idhini ya mahakama wala ripoti ya kuhalalisha au kudunisha ubora wa shehena hiyo.

Kwa mujibu wa wakili wa kampuni ya Patiala Danstan Omari, kesi kuhusu sakata hiyo sasa iko kortini ambapo wanasiasa hao wawili wameshtakiwa, mahakama ikiombwa iwaamrishe kufidia mmiliki wa kiwanda hicho hasara ya kuharibiwa kwa shehena hiyo.

Bw Nyutu aliteta kwamba wakati mitandao ya ufisadi na mabavu imepewa nafasi kutanda mashinani, wawekezaji hupoteza faida, wateja huhangaika na hata vibarua hukosa kiasi kwamba Jumapili ikifika, waumini hufika kanisani wakiwa hawana pesa za kuvumisha kazi ya Mungu.

Alisema wale waliopoteza hutatizika si haba wakimenyana kufa kupona kuepuka kutumbukia ndani ya lindi la umaskini na wakifika kanisani kazi yao ni kulia tu.

“Wao huja kanisani kumlilia Mungu asaidie viongozi wao wapate busara ya kiutawala nayo nchi ipate afueni. Wanaomba wao pia wapate pesa huku sisi watumishi tukihitajika kuwaombea tu tukiwa hatuna sadaka na kuwapa ushauri nasaha wa kustahimili hali,” akasema.

Alisema hiyo ndio sababu wanataka serikali izingatie mikakati yake pasipo kutoa mazingira ya ufisadi.

“Kwa sasa mimi nimechoka kuombea waathiriwa wa kubomolewa makazi na biashara, kufurushwa kutoka kwa mashamba yao kupisha miradi ya serikali itekelezwe huku fidia ikimezwa na mafisadi,” akasema.

Alidai ni uchungu watu kufungiwa biashara na wengine kukamatwa na kudaiwa hongo za kuwafanya wauze mali zao.

Mwanamume akiharibu pombe. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alisema msimamo wa makanisa ya kiasili ni kwamba “biashara ya baa sio haramu bali matendo ya wawekezaji pamoja na walevi ndio ya kumulikwa kwa msasa wa kisheria”.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu alisema vita hivyo dhidi ya baa na walanguzi wa mihadarati vimefika awamu muhimu sana ambapo ni lazima vifaulu lakini kwa msingi wa haki.

“Licha ya kuwa mimi ninaunga mkono vita hivyo, watekelezaji sheria na amri wajue ni hatia kukamata watu kiholela kwa lengo la kusaka hongo,” akasema Bw Nyutu.

Aliongeza kwamba ikiwa baa iko katika eneo ambalo halifai, inafaa tu kuamrishwa ifungwe lakini leseni isipigwe marufuku ili kumwezesha mwekezaji huyo kusaka nafasi ya kuhamia panapofaa.

Bw Nyutu alidai kwamba kumeingia fununu kwamba kuna wakusanyaji ushuru ambao wameingiwa na ubunifu wa kuwakamata wahudumu wa baa na pia walevi ili wakifikishwa mahakamani, watozwe faini ndipo uchumi wa taifa upate pesa za bajeti.

Bw Nyutu alisema ataunga mkono vita hivyo kwa msingi wa kuondoa pombe ya mauti mashinani na pia mihadarati “lakini sio katika ile hali ya kukandamiza wawekezaji wa baa na kuwaangazia kama wanaoshiriki biashara haramu”.

[email protected]