Habari Mseto

Wahubiri waomba makanisa yafunguliwe kwa zamu

April 16th, 2020 1 min read

Na JUSTUS OCHIENG

VIONGOZI wa kidini kutoka eneo la Nyanza sasa wanataka makanisa yafunguliwe na waumini wahudhurie ibada kwa zamu ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Viongozi hao wanasema kuwa, imani ya baadhi ya waumini imeanza kufifia baada ya kukosa kwenda makanisani kwa wiki kadhaa sasa.

Viongozi wa makanisa wanashinikiza kufunguliwa kwa makanisa huku serikali ikionya kuwa, virusi vya corona vimeanza kasambaa katika kaunti mbalimbali nchini.

Viongozi hao wa kidini chini ya Baraza la Makanisa katika eneo la Nyanza walimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuondoa marufuku ya kutoenda kanisani huku wakisema, maombi yatasaidia kupunguza makali ya virusi vya corona.

“Tumegundua kuwa imani ya baadhi ya waumini imeanza kufifia kwa kuwa wamekosa huduma ya kiroho ambayo walikuwa wakipata kila Jumapili,” wakasema viongozi hao wa makanisa kupitia taarifa iliyosomwa kwa niaba yao na mwenyekiti wa baraza hilo, Dkt Washington Ogonyo-Ngede jijini Kisumu.

Alisema: “Tunasihi serikali kuruhusu makanisa kote nchini kuendelea na ibada zao kwa zamu ili kuepuka msongamano makanisani.”

Taarifa hiyo ilitiwa saini na Dkt Ngede, Askofu Mkuu Julius Otieno, Patrick Ligawa, Maaskofu John Onyango Ober, Dkt William Abuka, Jasper Ogello na John Ongongá.

“Ili kumaliza hofu iliyo nchini, kuna haja ya kuuhubiri ujumbe wa matumaini,” akasema Dkt Ngede.

Serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu, ikiwemo mikutano ya ibada makanisani na harusi, kama njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona nchini.