Makala

Wahudumu baa waishi maisha ya juu kuliko mishahara yao

March 14th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

HALI ambapo wahudumu wa baa hasa wale wa kike hupata mshahara wa kiwango cha chini lakini wanaonekana wakiishi maisha ya juu kuliko pato lao, imezua gumzo mtaani.

Mwanadada Cecilia Wambui ambaye huuza pombe katika kilabu kimojawapo mjini Murang’a, hulipwa Sh7,000 kwa mwezi lakini anaishi nyumba ambayo kodi yake ni Sh8,000 kwa mwezi.

“Kando na kodi ya nyumba, nina watoto ambao ninawalea na kwa sasa wako katika shule ya msingi ya umma ambapo nauli yao ya pikipiki kwa siku ni Sh200,” asema Bi Wambui.

Bi Wambui anasema akijumuisha bila za stima na maji na kiasi fulani cha matumizi yake ya kibinafsi na zile pesa za kuwapa wazazi wake, bili yake ya kila mwezi ni Sh45,000.

Kuhusu vile yeye huishi na bajeti ya juu hata kuliko ya baadhi ya polisi, walimu, walinzi na wafanyakazi wa serikali za kaunti, Bi Wambui anasema “maisha ni kujipanga jinsi ambavyo Rais William Ruto hushinda kutukumbusha”.

Anasema ni mwanachama wa makundi mawili ya kustawishana kifedha na kimaendeleo.

“Huwa ninatoa Sh600 kwa makundi hayo na akiba yangu kwa miaka mitatu sasa huniwezesha kukopa Sh100,000 pasipo mdhamini yeyote,” aeleza.

Anasema kwamba kupata Sh600 kwa siku ni rahisi kwa kuwa “wateja wengi wakija kwa baa huninunulia pombe ambayo sikunywi.”

Anafichua kwamba yeye hurejesha pombe hiyo kwa kaunta na badala yake huwa anaweka pesa za kuzilipa mfukoni mwake hivyo basi kivyovyote vile “simnyimi mdosi wangu nafasi ya kuuza pombe hiyo”.

“Ninaweza tu nikamkosea mdosi wangu endapo wewe utakuja ununuliwe pombe halafu nikatae kukupa na nichukue pesa hizo. Hapo ndipo unaweza ukasema nimefanya dhuluma,” ajitetea.

Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kiambu Anne wa Muratha anasema wahudumu katika baa ni watu wa kujituma wanaostahili pongezi.

“Wengi wao ni wazazi wanaotilia mkazo elimu ya watoto wao na pia wanajaribu juu chini kusaidia wazazi wao nyumbani kwa kuwa mara nyingi huwa wametoka katika familia zisizojiweza,” asema Bi Wa Muratha.

Anawatetea huku akitoa wito kwa jamii isiwahukumu kuwa ni vibiritingoma.

“Kile ninachosema ni kwamba wahudumu hao huwa na ubunifu wa kipekee wa kuunda urafiki na kuingia kwa vyama vya ushirika, hatua zinazowapa fursa kujiendeleza kimaisha,” asema.

Kuhusu swala la mahusiano, mhudumu mmoja anasema hawafai kukaziwa sana maisha kwani pia wanajua kupenda na hutaka kupendwa. Yeye anajitambulisha tu kuwa anaitwa Alice.

Alice huhudumu katika baa moja ya mjini Thika.

“Hata sisi wahudumu wa baa tuko na haki ya kupendwa na huwa tuna wetu wa roho ambao huchangia bili zetu kukabiliana na haya maisha magumu,” asema Alice.

Kuhusu baadhi ya wahudumu kuwa na zaidi ya mchumba mmoja anasema huo ni uamuzi wa mtu binafsi “bora tu hakuna sheria inayovunjwa”.

Alice anazua utata akisema baadhi ya wanawake hawajui kutunza waume.

“Wewe usipochunga bwanako na umfuge nyumbani unatakaje? Ikiwa hana nidhamu na haheshimu ndoa yenu kiasi kwamba anakuja kwetu tumuonyeshe upendo huku naye akigharimia maisha yetu, sisi tutampokea tena kwa mikono miwili,” asema.

Lakini wanaume wengine huamini kwamba wahudumu hao hupata hela nyingi kupitia kupora walevi na hata katika visa vingine, kuwateka nyara waume wa watu kwa kutumia ndumba.

Martin Kiragu ambaye ni mteja wa baa mjini Makutano katika Kaunti ya Embu, anawatahadharisha wanaume.

“Ukilewa kiholela ndani ya baa ukiwa huna wa kukuchunga utajua baa ni jehanamu nyingine. Hao wahudumu watakupora, wakutapeli na wakupokonye hata viatu,” aonya.

Anaongeza utalipishwa bili kwa bei za juu na ujumlishaji wa bili uongezewe gharama nyingine kiharamu.

“Niliwahi kuingia kwa baa nikiwa na Sh40,000 na nikawa sina kitu siku iliyofuata. Hakuna vile ningekuwa nimekunywa pombe ya pesa hizo zote. Ukweli wa mambo ni kwamba niliporwa na wahudumu,” asema.

Naye Bw Tom Ikonya ambaye Novemba 2022 alitikisa dunia kwa huruma alipokiri vile aliporwa Sh800,000 na mwanamke ndani ya baa mjini Maragua katika Kaunti ya Murang’a, anasema kwamba “ningekuomba kwa hisani kuu uachane na mambo ya baa ikiwa huna nidhamu za kulewa”.

Bw Paul Kamau ambaye mwaka 2023 naye alipoteza Sh283,000 siku moja katika baa ya Maragua, anasema “mimi ninajua vile hao wahudumu huishi maisha ya juu kuliko mishahara yao”.

Anasema kwamba uchunguzi wa polisi kuhusu jinsi pesa zake zilivyopotea kutoka kwa akaunti yake ya simu ulifichua kwamba wahudumu wawili wa kike ndio walijitumia pesa hizo.

“Walijitumia pesa baada ya kunipa dawa za kunizubaisha na nikalala huku tayari wakiwa wamenihadaa hadi nikawapa nambari yangu ya siri ya akaunti yangu,” asema Bw Kamau.

Bw Kamau anasema kwamba “licha ya polisi kukamata wahudumu hao wawili na pia mwajiri wao kwa kuwa hela kiasi kiingine zilikuwa zimetumwa kwa nambari ya malipo ya baa hiyo, “sikupata pesa zangu”.

“Baadhi ya wahudumu katika baa ni hatari kwa pesa zako kuliko majambazi mtaani au polisi wanaodaiwa kuwa na mazoea ya kuitisha hongo kutoka kwa madereva barabarani,” adai.

Lakini Alice anasisitiza kwamba maisha ni kujipanga au upangwe.

“Unafaa ujue namna ya kuchunga jasho lako la sivyo, litamfaa mwingine kwa hiari yako,” asema.

Anawashauri wanaume kuchukua tahadhari na nidhamu ndani ya baa kwa sababu “hao unaona huko sio wazazi wako ambao watakuhurumia kwa mapenzi ya kukuzaa na kukulea”.

“Huko utakamuliwa hadi peni la mwisho bila huruma,” aonya.

[email protected]