Habari Mseto

'Wahudumu wa afya Mombasa hawana bima ya afya'

September 3rd, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Mombasa wanafanya kazi bila bima ya afya wakiendelea kuhatarisha maisha yao wanapokabiliana na janga la corona.

Haya yalifichuka kwenye mahojiano kati ya kamati ya bunge la seneti kuhusu corona na vyama vya madaktari na wahudumu wa afya.

Madaktari walifichua namna mwenzao, Dkt Biabu Adam, alikuwa mgonjwa na kulazimika kugharimia matibabu alipolazwa hospitali moja ya mmiliki binafsi.

“Ugonjwa huo ulisababisha nijifungue kwa njia ya upasuaji ya dharura. Nilishangaa kwamba bima yangu ya afya ilikuwa haijalipwa ilhali sikuwa na uwezo wa kusimamia gharama hiyo kwa wakati huo, ” alisema Dkt Adam kwenye barua aliyomwandikia afisa wa afya Dkt Khadija Shikely mnamo Julai.

Baada ya upasuaji huo, daktari huyo ambaye anafanya kazi katika hospitali ya wilaya ya Tudor alipewa bili ya Sh190,000.

Mwezi mmoja baadaye anang’ang’ana kulipa pesa hizo huku wenzake wakiendelea na mchango.

“Alidhania bima yake ya afya itasimamia gharama hiyo lakini tukagundua kaunti ilisitisha malipo. Inasikitisha kuwa madaktari na wahudumu wengine wa afya wanakabiliana na janga hili na hawana bima ya afya,” alisema naibu katibu wa chama cha madaktari nchini tawi la Pwani Dkt Niko Gichana.

Hii ni taswira ambayo inawakumba zaidi ya madaktari 100 na wahudumu wa afya ambao wanalalamika kuwa hawana bima ya afya.

Hata hivyo, serikali ya Kaunti ya Mombasa ilijitetea huku ikiilaumu hazina ya bima ya afya chini NHIF kwa kukataa kuwapa wafanyakazi hao huduma hiyo.

Afisa wa afya ya umma Kaunti ya Mombasa Bi Pauline Oginga akihutubia wahudumu wa afya kwenye uzinduzi wa mafunzo ya namna ya kudhibiti maambukizi ya corona miongoni mwao. Picha/ Winnie Atieno

Walisema NHIF inawalazimu kulipa Sh142 milioni kabla wapewe bima hiyo.

Zaidi ya wahumudu wa afya 42 waliambukizwa virusi hivyo kaunti ya Mombasa.

Gavana Hassan Joho alisema serikali yake ilitafuta njia mbadala kwa kuwapa wafanyakazi hao matibabu ya bure katika hospitali kuu ya Pwani.

“Tumejaribu kukabiliana na swala hili lakini kuna changamoto,” Joho aliiambia kamati hiyo.