Habari Mseto

Wahudumu wa afya Mombasa watishia kugoma

June 13th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Mombasa wametishia kuanza mgomo baridi kufuatia kucheleweshwa kwa mshahara wa Mei.

Madaktari na wauguzi walisema Ijumaa wamekuwa wakipitia hali ngumu kutokana na hali hiyo huku wakiendelea kutoa huduma za afya kwa wakazi wanapokabiliana na janga la corona.

Walimtaka Gavana Hassan Joho kutatua swala hilo mara moja la sivyo watagoma.

“Tunataka mishahara yetu ilipwe na marupurupu ya kupambana na Covid-19. Tumejitolea mhanga na hata kuhatarisha maisha yetu kuhudumia wakazi lakini tunatelekezwa na hatuthaminiwi na serikali hii. Tunahudumia Wakenya bila ya vifaa vya kujikinga na virusi vya corona,” alisema Dkt Niko Gichana mkuu wa chama cha madaktari tawi la Mombasa.

Akiongea na wanahabari nje ya hospitali kuu ya Pwani, Dkt Gichana alisema zaidi ya wahudumu wa afya 40 wamepata virusi vya corona wakiwa kazini.

“Tumechoka na unyanyasaji huu; familia zetu zinahangaika tukiendelea kuwa katika hatari ya maambukizi ya corona. Tunataka mazingira bora ya kufanya kazi,” alisisitiza.

Kwa upande wake, wa wauguzi, mwenyekiti wa chama chao cha kitaifa tawi la Bw Peter Maroko alisema wahudumu wa afya hawana hata nauli ya kwenda kazini.

“Hatuna nauli ya kwenda kazini, itabidi tusalie majumbani mwetu,” alisisitiza Bw Maroko.