Habari Mseto

Wahudumu wa afya na wagonjwa katika hospitali ya Thika Level 5 wanufaika na misaada

December 7th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SHIRIKA la NEST 360 limejitolea kupeana vifaa muhimu katika hospitali ya Thika Level 5 viwafae wagonjwa na wahudumu.

Afisa mkuu katika hospitali hiyo Dkt Jesse Ngugi, alisema shirika hilo lilitoa vifaa muhimu vya kusaidia wanawake wajawazito ambao wamelazwa katika hospitali hiyo.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh8 milioni vilisambazwa kwa wanawake waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.

Wakati huo pia shirika hilo liliwafaa wahudumu wa hospitali hiyo na vifaa vya kazi vya thamani ya Sh 2 milioni, huku pia wakipewa mafunzo jinsi ya kukabiliana na changa moto wanazopitia katika kazi yao.

“Tunashukuru shirika la NEST 360 kwa kazi nzuri ambayo wameonyesha ya kuijali hospitali yetu ya Thika Level 5. Hiyo ni ishara njema ambayo inastahili kupongezwa na wengi,” alisema Dkt Ngugi.

Wanawake waliojifungua watoto wachanga pia walinufaika na vifaa muhimu vya matumizi.

Dkt Ngugi alisema watazidi kushirikiana na wafadhili wengine kutoka sehemu tofauti ili waweze kunufaika pakubwa na misaada inayotolewa kila mara.

“Mahitaji ya wahudumu wa afya ni mengi hasa magwanda ya kazi yanahitajika sana na kwa hivyo tukipata yeyote aliye tayari kutufadhili tuko tayari kushirikiana naye,” alisema Dkt Ngugi.

Wiki moja iliyopita benki ya Equity ilitoa msaada wa vifaa vya kazi kwa wahudumu wa hospitali hiyo. Vifaa hivyo vilikuwa vya thamani ya Sh8 milioni.

Dkt Ngugi alisema madaktari wanapitia wakati mgumu wakiwa kazini ambapo cha muhimu kwao kwa sasa ni kupata magwanda ya kazi ili waweze kutekeleza wajibu wao jinsi ipasavyo.

“Hivi majuzi tulimpoteza daktari wetu Bi Jaquline Njoroge ambaye aliugua ghafla na kufariki. Tunajua ni kazi ngumu kuvumilia lakini kwa sababu ni wajibu wetu kutumikia wagonjwa hivyo ni sharti tufanye kazi yetu,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema tayari wametenga wagonjwa 20 ambao wanashukiwa kuwa na Covid-19 na kwa sasa wanaendelea kupata matibabu.

Alisema hivi karibuni watakubaliwa kurudi makwao watakapopata nafuu.

Dkt Ngugi alisema licha ya wahudumu wa afya kundelea kupitia masaibu mengi bado wanajizatiti na kuwahudumia wagonjwa.

“Madaktari ni watu waliokula kiapo kwamba la muhimu kwanza ni kuwatatumikia wagonjwa kwa vyovyote vile licha ya mambo mazito wanayopitia,” alisema Dkt Ngugi.