Habari Mseto

Wahudumu wa afya, wagonjwa wamlilia Uhuru

December 14th, 2020 1 min read

MARY WANGARI na KALUME KAZUNGU

WAHUDUMU wa afya wanaogoma wamemsihi Rais Uhuru Kenyatta kuvunja kimya chake kuhusu malamishi yao, wakisema kwamba mahitaji yao hayakujumuishwa katika ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Maafisa wa chama cha kutetea maslahi ya matabibu (KUCO) walisema watasusia kazi hadi malalamishi yao yatakaposhughulikiwa.

Maafisa hao walikashifu serikali kwa kutilia maanani zaidi BBI kuliko maslahi ya wahudumu wa afya walio mstari wa mbele kukabili janga la COVID-19.

“Kila siku wanasiasa wanazungumza kuhusu BBI, ambayo haijawapa wauguzi hata jambo moja waliloomba. Hadhi ya wahudumu wa afya ni muhimu zaidi ya BBI,” akasema Mwenyekiti wa KUCO, Wachira Peterson

“Huu ndio wito wetu mkuu kwa Rais Kenyatta, kwani kwa sasa ni wewe unayeweza tu kujibu masuala yetu. Unaangazia asilimia 80 ya BBI, tungefurahi iwapo juhudi sawia na hizo zingetumika kuhusu mgomo wa wahudumu wa afya,” alisema Bw Wachira.

Alisema kuwa serikali ya kitaifa isipoangazia masuala yao, hawatarudi hospitalini.

Walisema hayo huku wagonjwa wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma za matibabu.

Jumatatu, wakazi wa Kaunti ya Lamu walimuomba Rais Kenyatta kuwaonea huruma kwa kusuluhisha kwa haraka mzozo kati ya serikali na wahudumu wa afya ambao umechangia kulemazwa kwa huduma za matibabu kwenye hospitalini za umma nchini.

Wakazi hao walieleza wasiwasi kwamba iwapo mgomo huo hautasitishwa, huenda Lamu ikashuhudia maafa zaidi.

Walimsisitizia Rais Kenyatta kuwahurumia kwa kutatua mzozo uliopo ili wahudumu hao wa afya warejelee shughuli zao.

Said Bunu, ambaye ni mgonjwa aliyekuwa amezuru hospitali ya King Fahad mjini Lamu kutafuta tiba Jumatatu, alieleza masaibu ya kukosekana kwa huduma hospitalini kutokana na mgomo unaoendelea.

Mgomo huo umelemaza huduma katika hospitali za umma kote nchini.