Habari

Wahudumu wa afya watishia kuendelea na mgomo Mombasa

November 6th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

WAHUDUMU wa afya katika Kaunti ya Mombasa ambao wanahudumu chini ya serikali kuu wametishia kuendeleza mgomo hadi watakapopata haki yao.

Kati ya malalamiko walioyaorodhesha ni kutokuweko na wafanyakazi wa kutosha, kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupandishwa madaraka, kutokuwepo kwa vifaa vya kutosha vya kuwakinga dhidi ya maradhi ya Covid-19 na fedha za kuwasitiri dhidi ya hali ngumu kipindi hiki cha janga la corona.

Pia, walilalamikia kuweko kwa wafanyakazi wachache wanaolazimika kufanya kazi nyingi zaidi.

Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya hospitali kuu ya eneo la Pwani (CGPH), wahudumu hao ambao ni pamoja na wauguzi, maafisa walio katika kitengo cha kutoa huduma za kuwaekea wagonjwa damu na wale ambao huhudumu katika bandari, walidai kuwa wanataka marekebisho kadhaa yafanyike katika sekta hiyo.

“Tunataka haki yetu. Hatuna barakoa za kutosha na vifaa vingine vya kutulinda dhidi ya virusi vya corona. Pia hatujapandishwa vyeo tangu mwaka wa 1998,” alisema mhudumu mmoja katika sekta ya kuwaekea wagonjwa damu, Hellen Muranga.

Bi Muranga alidai kuwa viongozi wao wamewasilisha barua kadhaa kwa Wizara ya Afya lakini hawajapata majibu yeyote.

“Punda amechoka sasa! Tutagoma hadi tupate haki yetu. Tukipandishwa vyeo na malalamishi yetu yote yashughulikiwe, tutarudi kazini kwa mpigo,” akasema Bi Muranga.

Mhudumu mmoja wa afya katika bandari, Bw Dennis Muasi aliiomba wizara hiyo iwape fedha za kuwalinda dhidi ya makali ya maradhi ya Covid-19.

Katika bandari wahudumu hao ukagua mizigo na abiria wanaoingia nchini kupitia bahari la Hindi.

“Walitupa fedha hizo kwa miezi mitatu tu. Corona bado ipo, na  bado tunafanya kazi kwa hali hiyo ngumu; tunahitaji pesa hizo,” akasema huku akiongeza kuwa wafanyakazi wengine waajiriwe ili kazi itendeke ipasavyo.

“Wafanyakazi wengi wanakaribia kustaafu ilhali wengine wa kuchukua nafasi zao hawapo. Serikali inafaa kuajiri watu mapema ili wapewe mafunzo na kupata tajriba ili waweze kuchukua nafasi za watakaostaafu,” akasema Bw Muasi.

Muuguzi mmoja aliyejitambulisha kwa jina Emily aliilaumu serikali kwa kuwatelekeza, akidai kuwa wauguzi ni wachache, wanafanya kazi nyingi kwa saa nyingi na hata hawaezi kuenda mapumziko.

“Nafurahi kuwa katika mstari wa mbele kupigana na corona, lakini serikali haitujali tena. Tumechoka kuomba kila wakati. Mkitupigia makofi kwenye televisheni, haitoshi manake mahitaji yetu hamjayatimiza. Tunalazimika kujitenga na watoto wetu kwa hofu kuwa tutawaambukiza corona,” akasema Bi Emily huku akisisitiza serikali ijitahidi kuhakikisha wahudumu wa afya hawafariki kutokana na maradhi ya Covid-19.