Wahudumu wa baharini watakiwa kuzingatia sheria

Wahudumu wa baharini watakiwa kuzingatia sheria

Na KALUME KAZUNGU

NAIBU Kamishna anayesimamia Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi, Bw Michael Yator, amewataka wahudumu wote wa vyombo vya usafiri baharini watii sheria ili kuepusha ajali.

Bw Yator alisisitiza hasa kuhusu ubebaji wa abiria wengi kupita kiasi na mizigo kwenye maboti, hali inayoweza kusababisha maafa. Akizungumza katika hafla ya kufuzu kwa mabaharia 300 waliopokea mafunzo ya uendeshaji mashua na boti, alisema idara ya usalama eneo hilo iko macho ili kuona kwamba sheria za usafiri wa baharini zinaheshimiwa kikamilifu.

Mafunzo hayo yalikuwa yameandaliwa na Mamlaka ya Uchukuzi wa Baharini (KMA). Mkurugenzi Mkuu wa KMA, Bw Robert Njue, alisema mafunzo hayo ambayo yamekuwa yakitolewa pia kwa wahudumu wanaotumia Ziwa Victoria maeneo ya Nyanza na Magharibi, yamenuiwa kuboresha usalama katika uchukuzi wa majini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KMA, Bw Geoffrey Mwango, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo aliwataka manahodha kutilia maanani usajili wa vyombo vyao wanavyotumia kubeba abiria baharini ili kurahisisha shughuli za uokoaji endapo vyombo vyao vitapata ajali.

Naibu Gavana wa Lamu, Bw Abdulhakim Aboud aliahidi ushirikiano wa dhati kati ya serikali ya kaunti hiyo, KMA na wadau wengine katika kuimarisha usalama wa safari za majini Lamu.

  • Tags

You can share this post!

Korti yazuia Waluke kusafiri nje ya nchi

Polo ajifanya sonko kumbe kijijini ni hoi

T L