Habari

Wahudumu wa bodaboda Thika walia 'bima ya mteja ni mzigo'

June 14th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa bodaboda mjini Thika na Juja wamelalamikia hatua ya Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich, kuwataka wachukue bima ya wateja wao ili kuiendesha biashara hiyo.

Wamesema hiyo ni njia moja ya kuwanyanyasa kifedha kwa sababu tayari mapato wanayopokea kutoka biashara hiyo hayatoshelezi matakwa yao yote.

“Sisi kama wanabodaboda tunafanya kujikaza kisabuni na hii kazi yetu. Hata pesa ya kulipia bima hiyo hatujui itatoka wapi,” amesema Bw Njoroge Njau ambaye ni mhudumu wa bodaboda mjini Thika.

Ameongeza hata katika barabara wanahangaishwa na baadhi ya maafisa wa polisi hata kwa makosa madogomadogo na mengine ya kubebeshewa lawama bure. Alizidi kusema hiyo imewaweka katika kona mbaya kabisa.

Wahudumu hao wamesema hata barabara nyingi wanazopitia ni mbovu ambapo zinaharibu pikipiki zao.

“Utapata sisi kama wanabodaboda tunafanya kazi muda wa saa nyingi na mahitaji yetu ni mengi, ambapo hata tuna familia. Sasa ukipiga mahesabu ya kutafuta pesa ya kulipia bima ya mteja inakuwa ni vigumu kwetu,” amesema John Kimani, ambaye ni mwendeshaji bodaboda mjini Thika.

Anahofia pengine polisi wataanza kuwahangaisha kwa sababu ya mwito huo wa bima ambapo hata wengine watalazimika kujiondoa katika biashara hiyo.

Bodaboda mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tunajua wazi polisi wataanza kutuandama kila mara na katika hali hiyo wengine wetu watakuwa wakijificha wanapopatana na polisi njiani,” alisema Bw Kimani na kuongeza kwamba “maskini atazidi kuwa pale huku tajiri akizidi kuinuka.”

Mhudumu bodaboda wa Juja, Bw Peter Kamau naye amesema sasa ndipo wamekabwa koo na serikali kwa sababu itawabidi wafanye kazi ya ziada ili kupata pesa za kulipia bima hiyo.

Wamesema baada ya kusikia tangazo hilo la Rotich walishindwa kuamini masikio yao kwa sababu sio wahudumu wengi wamekata bima ya kawaida hasa katika maeneo ya mashinani.

“Matangazo hayo tayari yamewatia wengine wetu kiwewe kwa sababu hatuna uhakika kama tutafanikiwa kikamilifu kuchukua bima hiyo inayohitajika,” amesema Bw Kamau.

Baada ya waandishi wa habari kuzuru vituo tofauti vya wahudumu wa bodaboda, mjini Thika na maeneo ya karibu, walipata wengi wao wakiwa wamekusanyika kwa vikundu wakijadili jambo hilo kwa kina.