Habari Mseto

Wahudumu wa bodaboda wa kijiji cha Githogoro wamlilia Mungu

March 24th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANAHUDUMU wa bodaboda na mekanika kutoka kijiji cha Githogoro, Rwaka, Kaunti ya Kiambu mnamo Jumatatu walimrejelea Mungu ili aweze kuzima janga hili la Covid-19.

Walisema wanataka janga hilo lipite haraka ili waendelee na shughuli zao za kawaida kwani kibarua chao cha kila siku ni muhimu kwa maisha yao.

Wanabodaboda hao walisema mambo ni magumu kwao ambapo hata wateja wamepungua kwa kiwango kikubwa.

Kwa siku moja wanapata kiwango cha chini sana cha fedha.

Walisema wanaendelea kufuata maagizo yote yaliyowekwa ya kunawisha wateja wao kabla ya kuabiri pikipiki.

Walisema iwapo kazi zao zitasitishwa bila shaka familia nyingi zitaumia.

Kufuatia janga la Covid-19 wakazi wa Githunguri, Kaunti ya Kiambu wamehimizwa kuripoti mgeni yeyote aliyetua nchini akitoka ng’ambo..

Chifu wa Githunguri Bw Jesse Mugo ametoa mwito kwa wakazi wa eneo hilo kushirikiana pamoja ili kuangamiza janga hilo la virusi vya corona.

“Janga hilo limetuvamia sisi wote na ni vyema tupambane nalo kwa njia zote. Huu sio wakati wa kulaumiana lakini ni wakati wa kufanya jambo lifaalo kwa manufaa ya kila mmoja,” alisema Bw Mugo.

Alisema wakati huu kila mmoja anastahili kujisahili na kujituma kwa kupunguza kutembea kwingi ili pia kujizuia na virusi hivyo vinavyotetemesha kila mmoja ulimwenguni.

Mwishoni mwa wiki jana wakazi wa Thika walianza kurejea nyumbani mapema.

Uchunguzi uliofanywa umebainisha ya kwamba mwendo wa saa mbili za usiku, mji huo uligeuka kuwa mahame huku maskani nyingi za burudani zikiwa zimefungwa.

Walinda usalama ndio walionekana mjini wakipiga doria huku matatu zikiwa zinabeba wasafiri wachache; hasa wa kurejea nyumbani baada ya shughuli za kutwa nzima.

Hata hivyo, kutoka Jumatatu ndipo wafanyi biashara wengi wataanza kusikia uzito wa uchumi kudorora.

Wamiliki wa baa za burudani, mikahawa, na hata duka za jumla ndio watapata uzito huo kwani watu wengi wameanza kubaki nyumbani wakiendesha shughuli zao huko.

Wakati huo pia Kaunti ya Kiambu imefunga maskani zote za kucheza mchezo wa Pool na maeneo ya video yamefungwa.

Wazazi pia wamehimizwa kufanya juhudi kuona ya kwamba wanafunzi wanaendelea na masomo yao nyumbani badala ya kurandaranda ovyo kila mahali.

Kulingana na ilani iliyotolewa kutoka afisi hiyo ya kaunti wazazi walishauriwa kufuatilia mienendo ya wana wao na kuhakikisha wanabaki kwenye nyumba.