Habari Mseto

Wahudumu wa bodaboda waomba wajumuishwe katika kamati za usalama

September 22nd, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

WAHUDUMU wa bodaboda katika Kaunti ya Mombasa wakishirikiana na shirika moja la kibinafsi wamewasilisha mkataba wa makubaliano kwa idara ya usalama wakiiomba iwajumuishe katika kamati ya usalama katika maeneobunge.

Akizungumza na waandishi wa habari katika jengo la mikutano la Kanisa Katoliki la St Mary’s, Changamwe wakisherehekea Siku ya Amani Duniani, meneja mkurugenzi wa shirika la Stretcher’s Youth, Bw Dickson Okong’o alisema kuwa ni muhimu kila mdau muhimu ajumuishwe katika mazungumzo kuhusu amani na usalama.

Shirika hilo limekuwa likiwapa wahudumu wa bodaboda mafunzo kwa mwaka mmoja sasa kupitia programu iitwayo Inuka, ili kuhakikisha kuwa wanakuwa miongoni mwa sekta zinazosaidia kuimarisha usalama katika jamii.

Bw Okong’o alisema pia ni vyema kama baadhi ya wahudumu hao wangechaguliwa kama mabalozi wa Nyumba Kumi ili waweze kuripoti visa vyovyote vya uhalifu katika maeneo wanayoishi, kwa mafisa wa polisi.

“Bodaboda ni mojawapo ya sekta ambazo zimepanuka sana katika jamii na wakishiriki katika maswala ya usalama na amani, wataweza kumaliza dhana mbaya katika jamii eti wahudumu ni wahalifu,” akasema Bw Okong’o.

Naibu mwenyekiti wa chama cha wahudumu wa bodaboda eneo hilo, Bw Josephat Musyoka alisema kuwa uhusiano kati ya wahudumu hao na polisi umeimarika.

“Kupitia mafunzo ambayo tumepokea, wahudumu wengi sasa wanafuata sheria na pia wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa sekta nzima haivutwi nyuma na watu wachache ambao wanashiriki vitendo vya uhalifu,” akasema Bw Musyoka.

Bw Musyoka alisema kuwa katika eneo hilo wamesajili zaidi ya wahudumu 1,250 na wataendelea na shughuli hiyo, ili kuhakikisha wale ambao hawafuati sheria wanatambuliwa.

Alisema baadhi ya changamoto ambazo bado zinaikumba sekta hiyo ni kuongezeka kwa watu

“Baada ya watu wengi kupoteza kazi kwa sababu ya janga la corona, watu wengi walikimbililia sekta hii angalau wapate riziki. Hata hivyo, wengine hawataki kutii sheria lakini tutapambana nao. Pia, kuna watoto wa shule ambao walikuwa wameanza kazi ya bodaboda lakini tumewakomesha,” akasema.