Dondoo

Wahudumu wa hoteli wakomesha mlofa aliyezoea kula bila kulipa

April 13th, 2024 1 min read

BOMBOLULU, MOMBASA

Na JANET KAVUNGA

UJANJA wa jombi wa hapa wa kutolipia mlo aliotafuna hotelini nusura umtumbukize pabaya wahudumu walipomkabili wakitaka kumvua nguo.

Duru zinasema kuwa jamaa aliingia hoteli moja ya hapa akaagiza mlo na chai moto. Yasemekana kwamba baada ya jamaa kushambulia mlo, alitaka kuondoka kabla ya kulipa deni lakini mhudumu mmoja akamtaka alipe pesa kabla ya kuondoka. Jamaa alikataa kulipa na kudai kuwa angelipa siku iliyofuata.

Mhudumu aliposikia hayo alimrukia jamaa na kumshika shati, akawaita wenzake waliotishia kumvua nguo iwapo hangelipa.

“Utalipa bili. Ujanja wako utaisha leo,” mhudumu mmoja alisema huku akimvua shati. Jombi alipoona aibu iliyokuwa ikimkodolea macho, aliingia mfukoni mara moja na kutoa pesa za bili nzima.

***

Mke ashangaza kutumia simu ya mumewe kupigia mpango wa kando

MOMBASA MJINI

Na JANET KAVUNGA

MWANADADA wa hapa alijitakia makubwa kwa kutumia simu ya mumewe kumpigia mpango wake wa kando. Inasemekana demu alitaka kuwasiliana na mpango wake wa kando lakini akaishiwa na credo.

Mumewe alipokuwa aking’orota kitandani, demu alichukua simu yake akaingia bafuni na kumpigia mpenzi wake wa pembeni lakini akasahu kufuta namba.Mumewe alipopata nambari mpya katika simu yake aliipiga na ikajibiwa na mwanamume aliyemwita switi.

Kwa hasira, alimzushia mkewe vikali baada ya kung’amua alikuwa mchepukaji na akaapa kumsaka jamaa amkabili.