Habari Mseto

Wahudumu wa matatu wapuuzao kanuni za kuzuia corona kukamatwa Machakos – Kamishna

December 21st, 2020 1 min read

Na SAMMY KIMATU

WAHUDUMU wa matatu ambao watapuuza sheria za trafiki na kukosa kuzingatia kanuni za kuzuia msambao wa corona kabla, wakati na baada ya Sikukuu ya Krismasi watakamatwa.

Akiongea na wanahabari Jumapili, kamishna wa Kaunti ya Machakos, Bw Fredrick Ndunga aliwahimiza wahudumu hao kufuata sheria la sivyo, watakabiliwa na athari zake.

“Serikali haiwezi kukaa chii na kufumba macho huku raia wake wakifa kutokana na uzembe wa wafanyikazi wa matatu, Sheria zote lazima zizingatiwe,” Bw Ndunga alisema.

Alisema zaidi kuwa usalama umeimarishwa katika kaunti na kuongeza kuwa maafisa wote wa utawala katika kaunti na maafisa wote wa polisi ambao walikuwa kwenye likizo wameamriwa kurudi kazini.

Msimamizi huyo aliwauliza wananchi kutumia nambari ya dharura ya bure ya 988 kuripoti visa.

“Natoa wito kwa kila mwananchi kutuma ujumbe mfupi ukianza na neno Machakos na utume kwa 988 na kuonyesha eneo la tukio na aina ya kisa chenyewe,” Bw Ndunga asema.

Kando na hayo, alihimiza wenyeji kuzingatia kufauata maagizo ya Wizara ya Afya ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Bw Ndunga alibainisha kuwa hakuna mikusanyiko ya watu inayoruhusiwa wakati wa likizo na alionya kuwa polisi wameimarisha doria kutoka miji yote, vituo vya biashara hadi vijini. Kando na hayo, alisema msako mkali utafanywa kuwanasa wale watakaopatikana wakivunja maagizo ya corona sawia na waendeshaji baa zisizo na leseni.

“Vita dhidi ya vinywaji haramu vinaendelea kwa hivyo hakikisha hautapatikana upande usiofaa wa sheria na wasimamizi wetu wa sheria,’’ alionya.

Bw Ndunga aliwasihi vijana waachane na dawa za kulevya na waepuke marafiki wasiofaa na badala yake wazingatie shughuli za kuongeza mapato.

Aliwashauri pia waepuke kushawishiwa na wanasiasa kusababisha vurugu. Kwa wazazi, Bw Ndunga aliwaambia wafuatilie watoto wao wakati wa likizo na wawashirikishe kikamilifu nyumbani.

“Kila mzazi lazima ahakikishe mtoto wake yuko salama nyumbani na hapaswi kuwaruhusu watoto wao kurandaranda katika masoko wakati wa msimu wa sikukuu,” alishauri.