Habari Mseto

Wahuni wachoma kanisa

September 22nd, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WAUMINI katika kanisa moja lililoko Kaunti ya Kirinyaga wameachwa kwa mshangao baada ya kanisa lao kuvamiwa kisha kulipuliwa na genge la wahalifu.

Kanisa hilo kwa jina Full Gospel Life Mission lililoko eneo la Difathas liligeuzwa jivu baada ya bomu la petroli kutupwa ndani na majambazi kisha kuhepa. Hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa katika kisa hicho.

Huku azimio la shambulizi hilo likiwa halijajulikana, wakazi bado wamepigwa na butwaa na kujawa na hofu.

Kutokana na kisa hicho, waumini walilazimika kufanyia maombi yao nje. Mchungaji wa kanisa hilo, Isaack Kiringa alisema wamepoteza mali ya thamani kubwa.

“Tumepoteza mali ya thamani ya shilingi milioni moja na hakuna chochote kilichookolewa katika mkasa huo wa moto.” alieleza Bw Kiringa.

Aidha, aliwaomba walioshiriki katika tukio hilo kutubu.

“Sikudhania kwamba mtu anaweza kuichoma nyumba ya Mungu,” alisema Mchungaji Kiringa.

Kulingana naye, waumini 200 sasa hawana mahali pa kuabudia.

“Walitupa bomu la petroli kanisani na wakati moto uliwaka, waumini walijaribu kuuzima bila mafanikio. Ulichoma viti na kila kitu kilichokuwa kanisani.” aliongeza Bw Kiringi.

Aliwataka maafisa wa polisi kufanya uchunguzi ili waliohusika wachukuliwe hatua kali.

“Wanapigana na Mungu na hakika hawatashinda.” Alisema Bi Lydia Muthoni ambaye ni mwekahazina wa kanisa hilo.

Waumini walidai kuwa wamekuwa wakihudumu kwa Amani ila huenda watu wa nje wanaopinga mahubiri huenda ndio chanzo cha moto huo.

“Tukio hili ni la kwanza kutokea tangu miaka ya ukoloni,” Bi Muthoni alisema

Akithibitisha kisa hicho, mkuu wa polisi katika kaunti hiyo, Anthony Wanjuu alisema kuwa uchunguzi umeanzishwa baada ya kisa hicho na akatoa onyo kali kwamba, waliohusika watakamatwa na kuhukumiwa vilivyo. Wakazi walihimizwa kushirikiana na maafisa wa polisi katika kufanikisha kukamatwa kwa wahuni hao.