HabariSiasa

Wahuni wanataka kichwa na viungo vya mwili wangu – Didmus Barasa

February 14th, 2019 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa amemwandikia Spika wa Bunge Justin Muturi akitaka aongezewe walinzi akidai maisha yamo hatarini.

Akihutubia wanahabari Alhamisi katika majengo ya Bunge, Bw Barasa alisema kuwa amekuwa akipokea simu na jumbe kupitia baruapepe kutoka kwa watu wasiojulikana wakitaka kumuua.

“Katika barua hizo wamekuwa wakiniambia kwamba,….. ‘tunataka kichwa chako kidogo na viungo vingine vya mwili wako, nyamaza na ukome kutangatanga’,” akasema.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee alisema kuwa watu hivi majuzi watu hao hao pia walijaribu kumteka nyara mwanawe wa kiume ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Consolata, Nairobi.

“Nilipata simu kutoka kwa mwalimu wa mtoto wangu akiniambia kwamba mwanaume fulani alikuja shuleni humo akidai ametumwa kumchukua mwanafunzi huyo amrejeshe nyumba. Mwalimu aliposisitiza kunipigia simu kwanza, jamaa huyo akatoweka,” Bw Barasa akaongeza.

Aidha, alielezea kisa ambapo watu fulani walipatikana wakisukuma lango la boma lake kule Kimilili kana kwamba walikuwa wakitaka kuingia humo kwa nguvu. Walitoroka lakini mmoja wao aliyekamatwa na kusemekana kuwa alikuwa mlevi.

“Kando na hayo miezi mitatu iliyopita nilishambuliwa na watu wenye bunduki lakini nikaponea. Niliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha bunge ambapo mtu mmoja alikamatwa na kesi hiyo bado inachunguzwana na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Langata,” Bw Barasa akasema.

Mbunge huyo alitoa wito kwa DCI katika eneo bunge la Kimilili na Nairobi kuharakisha uchunguzi kuhusu tisho kwa maisha yake.

“Ombi langu ni kwamba maafisa hao watatekeleza wajibu wao ipasavyo na kuhakikisha mkuwa wahusika wote wametiwa mbaroni. Kufikia sasa naridhika na kazi yao lakini anataka Spika Muturi aamuru niongezewe walinzi zaidi,” akasema.

Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Bi Catherine Waruguru ambaye alikuwa ameandamana na Bw Baarasa pia alidai kuwa mwanasiasa mmoja, ambaye hakumtaja, amekuwa akimtishia maisha.

“Ningependa kumwambia kwamba ni mimi kiongozi niliyechaguliwa na wananchi na simwogopi yeyote. Nitaendelea kutekeleza wajibu wangu kwa nguvu zangu zote,” akasema Bw Waruguru.