Habari Mseto

Wahuni wanavyotumia vidosho kupora madereva wa matrela

February 27th, 2024 1 min read

NA RICHARD MAOSI

BAADHI ya madereva wa matrela ya masafa marefu wamewashutumu akina dada wanaojifanya makahaba, huku wakiwaibia vioo vya magari – side mirrors.

Kulingana na madereva hao, wizi huo unahatarisha maisha yao haswa wanapoendesha magari usiku.

Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali, kupitia mahojiano na baadhi ya waathiriwa, umebaini kwamba kumeibuka mtandao wa magenge ya wahuni wanaoshirikiana na wafanyabiashara wa ngono kuharibu vioo vya kuongoza madereva wa lori.

Juma Ali (sio jina lake halisi), mmoja wa madereva kutoka Mombasa hadi Malaba, mpakani mwa Kenya na Uganda, anasema kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi visa hivyo vimeongezeka.

Maeneo ambayo ni moto wa kuotea mbali ni kituo cha Kibiashara cha Maai Mahiu, Salgaa, Kikopey, Naivasha na Juakali katika barabara ya Eldoret-Kakamega.

“Katika kipindi cha miezi minane, nimeibiwa side mirrors mara mbili,” akasema.

Dereva wa pili ambaye alijitambulisha kwa jina Charles anasema alikuwa akisafiri kuelekea Mombasa mwishoni mwa 2023, lakini alipofika eneo la Mlolongo alikutana na akina mama wawili ambao walikuwa wamekwama njiani na alipowasaidia waligeuka kuwa waporaji.

“Waliomba msaada wa kufikishwa Kyumbi, Kaunti ya Machakos na tukakubaliana wanilipe Sh300,” anasema.

Lakini Charles alipofika Athi River alishikwa na usingizi mzito na alipoamka asubuhi alijikuta hajitambui.

Alipopata fahamu alijikuta akiwa amelala ndani ya gari ila vioo vya trela yake vilikuwa vimeng’olewa vyote.

Anasema kuanzia siku hiyo, jambo la kwanza anapokuwa ameegesha lori lake usiku hutafuta sehemu ambayo haina makahaba.

Lau sivyo hupaki palipo mlinzi ambaye atamsaidia kulinda lori usiku anapokuwa ameenda kupumzika.

Mnamo 2014 Mahakama Kuu ya Nairobi ilitoa siku 60 kwa serikali kuweka mikakati faafu ya usafiri nyakati za usiku.

Agizo hillo lilitolewa baada ya serikali kupiga marufuku usafiri wa mabasi na matrela nyakati za usiku kwa hofu ya kusababisha ajali nyingi hasa msimu wa Krismasi.