Habari Mseto

Waiga sauti za fisi ili kuiba mifugo usiku bila bughudha

July 28th, 2019 2 min read

Na PIUS MAUNDU

WAFUGAJI kutoka eneo la Malili, Kaunti ya Makueni wanaishi kwa hofu, kutokana na uvamizi wa wezi wa mifugo ambao wamekuwa wakitoa milio kama ya fisi ili kuwatisha kabla ya kuwavamia na kuwaibia.

Kulingana na Bw Wilson King’ele ambaye alikuwa kiongozi wa eneo hilo zamani, wezi hao wamekuwa wakiiga milio ya fisi kama njia ya mazungumzo wakati wa uvamizi wao, na kama mbinu ya kutisha wakazi.

“Tumegundua majuzi kuwa kila wakati tunapodhani fisi wametuvamia, mifugo yetu inaibiwa na kuchinjwa. Tumeacha kufuga mifugo mingi kutokana na hali hiyo,” akasema Bw King’ele, aliyesema amekuwa akifuatilia visa vya wizi wa mifugo kwa zaidi ya miaka kumi.

Visa hivyo vilianza mnamo 2007 wakati wakazi walianza kuishi huko, wakati huo wezi wakiwatoa mifugo kutoka mazizini usiku.

Baadaye, wezi walianza kuchinja wanyama katika vichaka karibu na wanapowaiba, kisha kubeba nyama.

Hata hivyo, wakazi wamelalamika kuwa wanaokamatwa kwa wizi wa mifugo wao huishia kuachiliwa katika mazingira yasiyofahamika, wakigundua kuwa kila kabla ya tukio la wizi, huwa kuna milio ya fisi.

Kufikia sasa, wezi hao wanasemekana kuiba ngombe 500.

“Tunashangaa ni fisi gani hawa tunaozungumza kuwahusu,” Bw King’ele akasema. Mzee huyo amekuwa akiweka orodha ya wakazi ambao wameibiwa mifugo yao, kila tukio lolote linapotokea.

Takriban wiki mbili zilizopita, Bw Winfred Musembi aliibiwa ndume wake wanne wa gharama ya Sh200,000, wakati idadi isiyojulikana ya wezi waliingia zizini na wakawatoa, kuwapeleka hadi vichaka vya karibu na wakawachinja.

Wakazi pamoja na polisi, hata hivyo, waliwafuata na wezi walipogundua wanawindwa wakaacha mizoga na kupotea. Maafisa wa uchunguzi walisema wanaamini mpango ulikuwa nyama hiyo ipelekwe katika gari lililokuwa likisubiri na kusafirishwe hadi jijini Nairobi.

Wakazi sasa wanawataka polisi kuwaruhusu kuwatupia laana iitwayo Kithitu wezi hao, ambayo inaogopwa sana, kutokana na hali yao ya kuwahangaisha.

Katika mkutano wa usalama ulioandaliwa wiki iliyopita, ilibainika kuwa wezi hao wamekuwa wakishirikiana na wasafirishaji wa nyama, hali iliyomfanya Kamishna wa kaunti hiyo Mohammed Maalim kupiga marufuku usafirishaji nyama usiku.