Habari Mseto

Waiguru aagiza kina mama watengewe vyumba vya kunyonyesha

October 23rd, 2018 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

GAVANA wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, ameagiza kuwe na vyumba vya kina mama kuwanyonyesha watoto wao katika makao makuu ya kaunti na katika bunge la kaunti.

Alitoa agizo hilo alipounga mkono hoja iliyowasilishwa katika bunge la kaunti wiki iliyopita na diwani maalumu Anne Wachera.

Bi Waiguru alisifu hoja hiyo na kumwagiza mkurugenzi wa masuala ya kiusimamizi katika afisi yake ahakikishe vyumba hivyo ni nadhifu.

Kwenye pendekezo lake, Bi Wachera anataka serikali ilazimishwe kutenga vyumba hivyo katika majengo ya umma na ya kibinafsi.

“Vyumba hivyo vinafaa kuwa katika hospitali, vituo vya kuabiri magari ya umma na hata katika vyoo vya umma. Hii itaongeza usafi na heshima,” akasema Bi Wachera kwenye mkutano wa wanawake wa Kirinyaga katika hoteli iliyo Sagana.

Anataka pia serikali iwe inasaidia wajane na mayatima kutatua mizozo ya urithi.

“Kunahitajika kuwe na mtaalamu katika masuala yanayohusu urithi ili kusaidia katika ugavi wa mali iliyomilikiwa na jamaa waliofariki. Wajane na mayatima hudhulumiwa na inahitajika wafunzwe kuhusu haki zao,” akasema.

Zaidi ya hayo, ametoa wito usambazaji wa maji safi uimarishwe vijijini na kuwe na hamasisho kuhusu maambukizi ya HIV ili kuepusha kutengwa kwa wanawake wanaougua Ukimwi.

“Baadhi ya wanawake wenye Ukimwi hushika mimba na hawajui wamgeukie nani. Kuna mambo yanayofanyika katika kaunti hii ambayo yanaweza kusaidia wanawake wapate ufahamu zaidi. Tunataka usaidizi kutoka kwa gavana,” akasema Bi Wachera.