Habari Mseto

Waiguru akaangwa kwa kudai changamoto eneo la Mlima Kenya si ukweli

November 22nd, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

GAVANA Anne Waiguru wa Kirinyaga alikosolewa vikali Jumatano kwa kudai kuwa malalamishi kuhusu ugumu wa kiuchumi katika ukanda wa Mlima Kenya ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi si ya kweli.

Bi Waiguru alitoa kauli hiyo Jumanne kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga, akisema kuwa madai kuhusu kudorora kwa sekta ya kilimo katika ukanda huo hayana ukweli hata kidogo.

Baadhi ya viongozi na wenyeji wa ukanda huo wamekuwa wakilalamika kuhusu kudorora kwa kilimo cha mazao kama majanichai, kahawa, miraa, mpunga na pareto huku wakiilaumu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kutochukua hatua za kutosha kuitatua.

Hata hivyo, Bi Waiguru alipuuzilia mbali madai hayo, akisema kuwa si eneo hilo pekee linalokumbwa na changamoto hizo.

“Matamshi kuhusu ugumu wa kiuchumi katika ukanda wa Mlima Kenya hayana ukweli hata kidogo, kwani hali ni sawa katika maeneo mengine nchini,” akasema Bi Waiguru, kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi walimkashifu vikali, wakisema kuwa yeye ndiye haelezi ukweli kuhusu hali ilivyo katika ukanda huo.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aliahidi kumtembeza gavana huyo katika eneo hilo, ili kumwezesha kuelewa kuhusu hali ilivyo.

“Kwa Bi Waiguru: Kinyume na kauli uliyotoa, malalamishi ya wakazi wa Mlima Kenya ni ya kweli. Wakazi haio wanataka maendeleo. Hali ya uchumi wa eneo hilo imedorora. Mazao tuliyitegemea kujijenga kiuchumi yameathirika, hata mpunga katika Kauntu ya Kirinyaga,” akasema Bw Kuria.

Akaongeza: “Kuna ukosefu wa maji katika kaunti zote kumi za eneo hilo. Vijana hawana ajira. Maziwa yananunuliwa kwa Sh17 kwa lita moja kwa kuwa baadhi ya kampuni za maziwa zinayanunua kwa Sh10 pekee nchini Uganda.”

Kando na hayo, Bw Kuria alisema kwamba sheria za kiuchumi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinatumiwa kuwahujumu wakulima kutoka Kenya.

Kauli za viongozi hao zinajiri huku migawanyiko mikubwa ya kisiasa ikiendelea kudhihirika katika ukanda huo kati ya mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’.

Hii ni licha ya kikao cha viongozi kilichoitishwa na Rais Kenyatta katika eneo la Sagana, Kaunti ya Nyeri kujaribu kukabili migawanyiko miongoni mwa viongozi.

Baadhi ya wanasiasa wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakidai kwamba mkutano huo haukufaulu kwani haukuangazia changamoto za kiuchumi zinazolikabili eneo hilo.

Miongoni mwa wale wamejitokeza wazi kuukosoa wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Cate Waruguru (Laikipia), Kimani Ngunjiri (Bahati) kati ya wegine.