HabariSiasa

Waiguru alivyoingiza Raila 'boksi'

June 15th, 2020 2 min read

Na CHARLES LWANGA

CHAMA cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, kimesema kuwa kitasimama kidete kumtetea Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru anayekabiliwa na hoja ya kumtimua mamlakani kwa madai ya ufisadi na utumizi mbaya wa mamlaka.

Kiranja wa wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed alitangaza jana kuwa ODM kitamtetea Bi Waiguru kwa hali na mali kwa kuwa wamegundua “anaonewa”.

Alisema kuwa chama cha ODM kinathamini uongozi wa wanawake na kitawapatia nafasi sawa.

“Kuna baadhi ya watu ambao wanaamini wanawake hawawezi kuongoza na sisi kama chama cha ODM tunaamini uongozi wa wanawake na tutasimama naye kwa sababu wanawake wanafaa kupewa nafasi sawa uongozini,” akasema akiwa Tana River.

Juma lililopita, madiwani wa kaunti ya Kirinyaga walipitisha hoja ya kumbandua Bi Waiguru kwa madai ya ufisadi na utumizi mbaya wa mamlaka.

Seneti imependekeza kamati ya maseneta 11 kushughulikia madai hayo, ingawa uamuzi unatarajiwa kufanywa kesho kuhusu iwapo watadumisha kamati, au kutumia kamati inayohusisha bunge lote la Seneti.

Mbunge huyo wa Suna Mashariki, alisema hayo alipotembelea waathiriwa wa mafuriko eneo bunge la Garsen, Kaunti ya Tana River ambapo aliandamana na Mbunge wa eneo hilo Ali Wario, Mbunge wa Galole Said Hirbae na Mbunge wa Isiolo Rehema Jaldesa.

Mbunge huyo pia alionekana kuashiria kuwa kinara wa chama hicho alikutana na Bi Waiguru kama ilivyoripotiwa magazetini akisema kuwa wana haki ya kukutana na kujadili.

“Kwani Waiguru na Raila wakikutana kuna shida gani? Waiguru ni gavana na Raila ni kiongozi humu nchini na wana haki ya kukutana mahali popote wakati wowote hapa nchini,” alisema.

Lakini huku chama hicho kikipanga kumtetea, wabunge watatu watatu wa Chama cha Jubilee (JP) katika Kaunti ya Kirinyaga, wanataka hoja ya kung’olewa mamlakani kwa gavana huyo kujadiliwa na Seneti nzima.

Wabunge Kabinga Thayu (Mwea), Gichimu Githinji (Gichugu) na Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati) walisema kuwa ili wakazi wa kaunti hiyo waridhike, lazima maseneta wote washirikishwe kwenye mjadala kuhusu hoja hiyo.

Wakiongozwa na Seneta Charles Kibiru, wabunge hao walipinga mpango wa mchakato huo kuendeshwa na Kamati Maalum ya Seneti yenye wanachama 11.

Walieleza hofu kuwa huenda kamati hiyo ikawa na mapendeleo,.

Wabunge hao walisema kuwa wakazi wa Kirinyaga walizungumza kupitia madiwani wao, hivyo Seneti inapaswa kuheshimu uamuzi wao.

“Suala la Bi Waiguru linapaswa kuendeshwa na Seneti kama ilivyoendesha hoja dhidi ya aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinard Waititu ili kuhakikisha watu wa Kirinyaga wamepata haki,” akasema Bw Kabinga.

Pia walimwonya Kiranja wa Wengi, Bw Irungu Kang’ata dhidi ya kuendesha mpango wowote wa kumwokoa Bi Waiguru.

Bw Wario alisema anaunga mkono hatua ya vyama kuwaadhibu wanasiasa waasi ambao wamekuwa wakiuka amri ya vyama na kwenda kinyume na maagizo ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Ninaunga mkono hatua ya kuwaadhibu wanasiasa waasi kwani tunataka siasa ya maendeleo na amani kupitia kwa maridhiano ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, ” alisema.

Naye Bw Hirbae aliwakashifu viongozi wanaoeneza chuki katika kaunti ya Tana River akisema huenda yakaleta vita.

“Hapa Tana River haswa Tana Delta tumeshuhudia amani kwa miaka mingi ambapo jamii ya Pokomo imekuwa ikiishi pamoja na jamii ya Oroma bila balaa, na hatutakubali viongozi waanze siasa ya kugonganisha jamii,” akasema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa wanawake Isiolo aliwasihi wakazi waishi kwa amani na kukumbatia maridhiano.