Habari MsetoSiasa

Waiguru atishia kumshtaki King Kaka kuhusu wimbo wa ‘Wajinga Nyinyi’

December 16th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

GAVANA wa Kirinyaga Ann Waiguru ameagiza msanii wa muziki wa kufokafoka Kennedy Ombima, almaarufu King Kaka au Kaka Sungura, kuondoa katika mtandao wa Youtube wimbo wake wenye jina la ‘Wajinga Nyinyi’.

Bi Waiguru pia anataka King Kaka amwombe msamaha kwa kumhusisha na sakata ya wizi wa mamilioni ya fedha katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) katika wimbo huo alioupakia katika Youtube, Jumamosi.

Gavana huyo, kupitia kwa kampuni ya kutoa huduma za kisheria ya Kiragu Wathuta, anasema kwamba wimbo huo unamchafulia sifa.

Anataka King Kaka kuondoa wimbo huo mtandaoni kisha aombe msamaha kwa kipindi cha saa 48, la sivyo atamshtaki.

“Kwa niaba ya mteja wetu, tunakuagiza kuomba msamaha na kuondoa video hiyo mtandani katika kipindi cha saa 48 tangu kupokea barua hii,” ikasema barua hiyo aliyoandikiwa King Kaka.

Maneno ya wimbo huo yaliyomkera Bi Wauguru yanasema: “Ati Waiguru ako kwa ofisi na stori ya NYS tulisahau, biro (kalamu) moja alibuy (alinunua) kwa 8 thao (Sh8,000) na biro tunanunuanga mbao (huwa tunanunua kwa Sh20) …”

Bi Waiguru anasema wimbo huo umemfanya kuonekana kama kiongozi ambaye ni fisadi na alihusika katika wizi wa fedha za NYS; madai ambayo si kweli.

Anasema kuwa wimbo huo umemfanya kuonekana mtu ambaye maadili yake yanatiliwa shaka na hafai kushikilia wadhifa wowote katika afisi ya umma.

“Unafaa kufahamu kuwa licha ya uchunguzi wa kina, mteja wetu hajawahi kushtakiwa mahakamani kuhusiana na sakata ya wizi wa fedha za NYS au sakata yoyote ile. Kadhalika, hakuna ushahidi ambao umewahi kupatikana au kuwasilishwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC),” anasema Bi Waiguru.

Aliongeza kuwa wimbo huo umemsababishia hasara kubwa na umemchafulia jina.

Bi Waiguru anadai kuwa msanii huyo analenga kutumia jina lake kujitafutia umaarufu.

Mara baada ya kutoa wimbo huo, Jumamosi, King Kaka alimiminiwa sifa si haba na Wakenya katika mitandao ya kijamii.

Katika wimbo wake, King Kaka, anazungumzia kuhusu ufisadi ambao umekita mizizi katika jamii ambapo wapigakura wanawachagua ‘wezi’ wanaopora fedha zao za ushuru.

Msanii huyo pia anashambulia Wakenya kwa kushambuliana kwa msingi wa kikabila.

Mkurugenzi wa Bodi ya Kutathmini Filamu nchini (KFCB) Ezekiel Mutua amempongeza King kwa wimbo wake ‘Wajinga Nyinyi’.

Kulingana na Dkt Mutua, watu wanaohisi kwamba wamekerwa na wimbo huo waende mahakamani na bodi yake haitaagiza uondolewe kutoka Youtube.

Wakili wa masuala ya kikatiba Ahmednasir Abdullahi aliahidi kumsimamia King Kaka mahakamani endapo atashtakiwa.

“Umesema ukweli mtupu. Ukihitaji wakili endapo utapelekwa mahakamani kwa kusema ukweli, usisite kunieleza #WajingaNyinyi” akasema wakili huyo kupitia mtandao wa Twitter.

Abdullahi ambaye alimwakilisha Gavana Waiguru alipofika mbele ya EACC kuhusiana na sakata ya NYS huenda akajipata katika njiapanda iwapo kiongozi huyo wa Kirinyaga atamshtaki King Kaka.