Habari MsetoSiasa

Waiguru, Aukot wakwaruzana tena kuhusu Punguza Mizigo

September 11th, 2019 1 min read

NA LEONARD ONYANGO

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru na kiongozi wa Thirdway Alliance, Ekuru Aukot Jumatano waliendelea kurushiana cheche kali za maneno kuhusu Mswada wa Punguza Mizigo.

Wawili hao walianza kuzozana kupitia mitandao ya kijamii mara tu baada ya Bunge la Kaunti ya Kirinyaga kutupilia mbali Mswada wa Punguza Mizigo unaolenga kupunguza idadi ya wabunge.

Bi Waiguru alitaja mswada huo kama ‘aibu’. Gavana huyo wa Kirinyaga alidai kwamba, Bw Aukot alinufaika na sakata ya wizi wa fedha katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).

Bw Aukot, alijibu kwa kusema kuwa Bi Waiguru hafai kuzungumzia masuala ya uadilifu.

Kabla ya kutupiliwa mbali kwa mswada huo Jumanne, majibizano makali yalizuka miongoni mwa madiwani wa Bunge la Kaunti ya Kirinyaga.

Hali hiyo inaonekana kuwa pigo kwa Dkt Aukot, ambaye amekuwa akizuru mabunge ya kaunti mbalimbali akiupigia debe mswada huo.

Bi Waiguru alifurahia hatua hiyo, akiwapongeza madiwani kwa kutoupitisha.

“Nina furaha kubwa kuwa mswada huo haukupita,” akasema Bi Waiguru, ambaye ametangaza kuunga mkono Jopo la Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Gavana huyo alisema kuwa mswada huo hauwafai Wakenya, akiyaomba mabunge mengine kuuangusha.

Alisema ataendelea kupigia debe jopo la BBI, ambalo sasa linatayarisha ripoti maalum baada ya kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya.

Hali ya taharuki ilitanda bungeni humo baada ya Kiongozi wa Wengi anayekumbwa na upinzani Bw Kamau Murango kukosa kuanzisha kikao cha kuujadili katika muda uliowekwa.

Baada ya muda, Bw Murango aliamka na kusoma mswada, huku akimwita diwani wa wadi ya Murinduko Bw Evans Ndege kuendesha kikao cha kuujadili.

Jana, mswada huo ulijadiliwa katika Bunge la Busia ambapo alikanusha kwamba haujafadhiliwa na Naibu wa Rais William Ruto.

Bw Aukot alisema madai kwamba mswada huo umefadhiliwa na Dkt Ruto huenda yakawa pigo kwa Punguza Mizigo.