Habari Mseto

Waiguru hatarini kufungiwa nyumba

November 18th, 2020 2 min read

Na SAM KIPLAGAT

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru anakabiliwa na hatari ya kufurushwa katika makazi yake ya kifahari mtaani Kitisuru jijini Nairobi kwa kukosa kulipa malimbikizo ya kodi ya Sh44.5 milioni.

Bi Waiguru alielekea kortini na kutaka itoe amri ya kuzuia kampuni ya Kihingo Village iliyostawisha makazi hayo dhidi ya kumfurusha. Kampuni hiyo imemtaka gavana huyo alipe Sh80 milioni au aondoke baada ya kukiuka makubaliano yaliyoafikiwa mnamo Septemba 25, 2015 na pande zote mbili.

Hata hivyo, Waziri huyo wa zamani wa Ugatuzi alijitetea akisema kuwa alishalipa Sh40 milioni pesa taslimu na alikuwa ameafikiana na benki ya KCB kumpa mkopo wa Sh40 milioni ili alipe kiasi kilichosalia. Ingawa hivyo, mkopo huo bado haujatolewa kutokana na kutokamilika kwa makubaliano akilaumu kampuni hiyo kwa kutowasilisha stakabadhi hitajika benkini.

Suala hilo linazingirwa na utata zaidi baada kampuni ya Kihingo kukanusha kuwa ilipokea fedha kutoka kwa Bi Waiguru huku ikimrejelea kama mpangaji badala ya mmiliki wa makazi hayo.

Aidha kampuni hiyo tayari imeteua madalali wa Chardor kuweka mali ya gavana huyo mnadani iwapo atakosa kulipa kodi hiyo ya miaka mitano iliyopita.

“Naomba korti hii itoe amri ya kuzuia kampuni ya Kihingo kumfurusha mteja wangu kutoka kwa makazi yake. Athari ya kutimuliwa kwake itakuwa mbaya ikizingatiwa anaishi huko na familia yake,” wakili wa Bi Waiguru, Bw Waweru Gatonye akaeleza mahakama.

“Pia amri hiyo itazuia kampuni ya Kihingo kutaka malipo ya kodi ambayo ni kinyume cha sheria na inakiuka makubaliano ya awali,” akaongeza.

Jaji Elijah Obaga alitoa amri ya muda inayozuia kampuni hiyo kumfurusha Bi Waiguru kwenye makazi hayo lakini akataka pande zote zitatue zenyewe utata unaohusu kodi.

Hata hivyo, gavana alisema uamuzi unaowataka kutatua wenyewe malipo ya kodi huenda ukachangia kampuni hiyo inayohusishwa na mbunge wa zamani wa Tetu Ndung’u Githenji kumtimua. Korti imeamrisha pande zote kwenye kesi hiyo zifike mbele yake mnamo Februari, 2021 wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo.

Gavana Waiguru anasema alinunua nyumba hiyo na kudai kulipa Sh40 milioni miezi miwili kabla ya kujiuzulu kama Waziri wa Ugatuzi mnamo 2015. Hii ni kufuatia sakata ya ubadhirifu wa mabilioni ya fedha zilizotengewa miradi ya NYS kwenye wizara hiyo.

Bw Gatonye pia alisisitiza kuwa lengo la kampuni ya Kihingo ni kumsawiri Bi Waiguru kama mtu asiyelipa kodi na asiyekuwa na maadili licha ya hadhi yake katika jamii.

“Ikizingatiwa hadhi yake kama gavana, kumsawiri kama asiyelipa kodi itafanya umma watilie shaka maadili yake,” akaongeza wakili huyo maarufu.

Kupitia kampuni ya uwakili ya Githuki King’ara, kampuni ya Kihingo ilitishia kumfurusha na kuuza mali ya gavana huyo, ikidai haiwezi kumruhusu kuishi kwa nyumba isiyo yake bila kuilipia kodi.

“Mteja wetu hawafahamu makubaliano na mteja wako ambapo alipewa miaka mitano kumaliza malipo ya nyumba. Ukiwa na nakala ya makubaliano hayo, naomba ututumie,” akaongeza.