Waiguru, Ngirici wazidi kuonyeshana ubabe

Waiguru, Ngirici wazidi kuonyeshana ubabe

Na WANDERI KAMAU

MVUTANO wa kisiasa kati ya Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga na Mwakilishi wa Wanawake, Bi Wangui Ngirichi, unaendelea kuchacha wawili hao wakiwania tiketi ya chama cha United Democratic Alliance UDA cha Naibu Rais William Ruto.

Wadadisi wanasema kwamba mvutano kati ya wawili hao, unatarajiwa kuendelea kutokota kabla ya uteuzi wa chama hicho.

Hii ni licha ya Naibu Rais William Ruto kuonekana jana kuwarai wawili hao kudumisha umoja wa kisiasa.

Kabla ya Dkt Ruto kuwasili jana katika kanisa la Kianglikana la All Saints (ACK), Kianyaga, Bi Waiguru alidai “kupokea vitisho” kutoka kwa polisi.

Hali hiyo ilitajwa kuchangiwa na taharuki kubwa ya kisiasa iliyokuwepo kati ya kambi za kisiasa za Bi Waiguru na Bi Ngirichi, ambapo wote wametangaza nia za kuwania ugavana katika kaunti hiyo mwaka ujao.

“Afisa Mkuu wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) katika eneo la Kianyaga amewaagiza wafanyakazi wangu kufika katika afisi za idara hiyo ili kuhojiwa. Anatishia kuwakamata kabla ya Dkt Ruto kuwasili,” akalalama Bi Waiguru.

Kabla ya hapo, vijana kadhaa walifanya maandamano huku wakichoma mavazi yenye nembo za Bi Waiguru.

Walitishia kuvuruga ziara ya Dkt Ruto, ikiwa Bi Ngirichi “hangejumuishwa ifaavyo” kwenye ziara hiyo.

Hata hivyo, Bi Ngirichi alimlaumu Bi Waiguru kwa “kupanga” njama hizo kimakusudi ili kumharibia sifa.

Ubabe wa wawili hao ulianza siku kadhaa kabla ya jana, ambapo wote waliweka matangazo makubwa katika mitandao ya kijamii kumwalika Dkt Ruto.

“Ninamwalika Dkt Ruto kukutana na kutangamana na wakazi wa Kirinyaga. Chaguo lao ni chama cha UDA,” yakaeleza matangazo yaliyowekwa na wawili hao kwenye mitandao ya kijamii.

Ingawa Dkt Ruto aliandamana na wawili hao sambamba kwenye mikutano aliyohutubu na kuwapa nafasi sawa kuhutubu, wadadisi wanatabiri kwamba ubabe huo utaendelea kutokota.

Katika siku za hivi karibuni, Bi Waiguru amejipata lawamani kutoka kwa baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo, baada ya kumrai Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho.

Bi Waiguru amekuwa akimlaumu Dkt Kibicho kwa “kujiingiza” katika siasa za kaunti hiyo, ilhali yeye ni mtumishi wa umma.

“Rais Kenyatta anapaswa kuwafuta kazi maafisa wa serikali ambao wamesahau kazi yao na kuingilia siasa. Ikiwa wameshindwa na kazi yao, basi wajiuzulu waanze kufanya kampeni,” akasema Bi Waiguru, alipoandamana na Dkt Ruto katika Kaunti ya Embu wiki iliyopita.

Dkt Kibicho amekuwa akionekana kudumisha ukaribu na Bi Ngirichi.

“Taswira tunayoona kwa sasa ni ya mzozo ambao hautaisha hivi karibuni. Yatakuwa ni marudio ya taswira sawa iliyoshuhudiwa 2017 kati ya Bi Waiguru na kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua. Ni mvutano unaoweza kuendelea hata baada ya uchaguzi wa ugavana kukamilika,” asema Dkt Geoffrey Sang’, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

You can share this post!

Mbunge akanusha kuhamia UDA

Jinsi ya kuandaa biriani ya nyama ya ng’ombe

T L