Kimataifa

Waikosoa serikali ya Zimbabwe kwa kuzima 'maandamano ya haki'

August 22nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

POLISI nchini Zimbabwe wamepiga marufuku maandamano ya kupinga serikali yaliyokuwa yamepangwa kufanyika jijini hapa huku serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa ikiendelea kukashifiwa kwa ‘uongozi mbaya’.

Maandamano hayo yaliyopangwa na chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) ni ya tatu kuzimwa ndani ya muda usiozidi wiki moja.

Wiki jana, polisi walizima maandamano katika jiji kuu Harare na ule mji wa pili kwa ukubwa, Bulawayo

Kuanzia Jumanne hadi jana mamia ya polisi waliwekwa katika barabara kuu za jiji la Gweru tayari kukabiliana na wafuasi wa upinzani watakaokiuka amri hiyo.

Kwenye taarifa, MDC ilitaja hatua hiyo kama sio tu “marufuku dhidi ya siasa za kiraia bali kutangazwa kwa hali ya hatari kinyume cha sheria,”

“Amri kama hii inayotumiwa kuhujumu haki za kidemokrasia na uhuru wa kijieleza inakwenda kinyume na katiba ya nchini yetu,” taarifa hiyo iliongeza.

Naye Naibu Rais wa MDC Tendai Biti alisema, kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, “vitendo vya serikali ya Mnangagwa ya kupiga marufuku maandamano ni sawa kupiga marufuku MDC na kusimamisha matumizi ya katiba kwa muda bila idhini ya raia wa Zimbabwe.”

Lakini aliahidi kuwa “tutaendelea kukabiliana nao kwa njia ya amani na inayokubalika kikatiba.”

Maandamano hayo yanalenga kuishutumu serikali na kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi katika hilo lililo kusini wa Afrika.

Biashara

Mnamo Jumanne, shughuli za kibiashara zilikwama jijini Gweru baada ya wenye maduka kufungwa biashara zao. Nao polisi waliokuwa wamejihami kwa marungu na vitoa machozi walionekana wakizunguka katika barabara za jiji hilo mchana kutwa kuzuia maandamano.

Na mnamo Ijumaa wiki jana polisi walitumia vitoa machozi na marungu kukabiliana na waandamanaji waliokaidi amri ya serikali na kujitikoza barabarani.

Takribani watu 12 walijeruhiwa katika makabiliano hayo.

Mabalozi wa Muungano wa Ulaya (EU), Australia, Canada na Amerika wameitaka serikali kutotumia nguvu kupita kiasi kukabaliana na waandamanaji.

Serikali ya Mnangagwa iliingia mamlakani kwa ahadi ya kuboresha uchumi na kurejesha uhusiano wa Zimbabwe na mataifa ya Magharibi lakini inaonekana kuwa hali inarejea kama ilivyokuwa wakati wa enzi ya Robert Mugabe.