Habari Mseto

Waililia serikali kuwanasua kutokana na minyororo ya pombe na kamari

April 19th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

WAKAZI wa kijiji cha Turi, Molo katika kaunti ya Nakuru wanalilia serikali kuwakomboa kutokana na mzigo mkubwa wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana na wazee, ambao wanasema unatishia kuangamiza kizazi.

Wakazi hao wamelalamika baada ya zaidi ya vijana watano kufariki ndani ya kipindi cha miezi miwili iliyopita katika hali tatanishi, kwenye visa vilivyohusishwa pakubwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Hii ilikuwa baada ya kijana mmoja kupatikana akiwa ameaga dunia siku ya Jumatano katika kijiji hicho, baada ya kudaiwa kubugia kileo bila kula.

Ni katika kijiji hicho ambapo mtoto wa darasa la sita alijitia kitanzi wiki chache zilizopita baada ya kupora Sh100 za babake akacheze Kamari, na kuwacha ujumbe nduguze wapikiwe chapatti siku ya mazishi.

“Eneo hili la Turi limekuwa na visanga kwa miezi miwili iliyopita, tumepoteza kama wanaume watano katika vifo tatanishi. Kuna wawili wa umri mdogo wamejiua manyumbani mwao,” akasema Bw Ndirangu, mkazi wa kijiji hicho.

Mzee huyo alisema kuwa kijiji hicho kimepoteza wazee kwa vijana katika hali zisizoeleweka.

“Huu msimu wa mvua umepita na vijana wengi kwani wana makazi mabaya na hawakuli vyema. Wengi wananyeshewa wakiwa walevi na wanaaga kutokana na baridi kwa kukosa pa kujikinga,” akasema Bw Ndirangu.

Mkazi mwingine naye alilaumu utumizi wa dawa za kulevya kuwa umezamisha takriban asilimia 80 ya vijana wa eneo hilo, akitaka viongozi waliochaguliwa kuchukua hatua kuokoa hali.

“Vijana wadogo wanafariki kwa ajili ya pombe, kama asilimia 80 ya vijana wameingilia pombe na dawa nyingine za kulevya. Japo wengi wangependa kujikomboa kutokana na ulevi, hakuna mielekezo myema ya kuwaokoa walioadhirika,” akasema mwalimu huyo, akiongeza kuwa.

Kama kuna lolote ambalo serikali inaweza kufanya ili kuwakwamua walioadhirika waachane na matumizi ya dawa za kulevya itasaidia sana.”